Na Paul Christian.
Mbunge wa Kigoma mjini Zuberi Zitto Kabwe
ameihoji serikali ni lini itawakamata na kuwafikisha mahakamani wabadhirifu wa
shilingi bilioni 28 za wakulima wa Tumbaku mkoani Tabora uliofanywa na viongozi
wa Chama Kikuu Cha Ushirika wa wakulima wa Tumbaku kanda ya Magharibi WETCU na wengine.
Kabwe ametoa hoja hiyo leo bungeni mjini
Dodoma wakati akiuliza swali la nyongeza ambapo amesema mwaka 2013 Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali CAG alitoa taarifa ya upotevu wa fedha za wakulima wa Tumbaku wa mkoa wa
Tabora.
Ameongeza kuwa, "aliyekuwa Rais katika serikali
ya awamu ya Nne alikwenda Tabora na kuagiza viongozi wa WETCU na wahusika wote wa
ubadhirifu ule wakamatwe mara moja na kufikishwa mahakamani lakini mpaka leo
hii hakuna ambaye amekamatwa wala kufikishwa mahakamani."
Kabwe amesema, "wakulima kupitia vyama vyao vya
msingi inabidi walipe fedha zile bilioni 28, serikali ya awamu ya Tano
inachukua hatua gani dhidi ya watu hawa ambao wamewaibia wakulima wa Tumbaku na
kuwafanya waendelee kuwa masikini licha ya kwamba wanajitahidi kulima mwaka
hadi mwaka."
Akijibu swali hilo la nyongeza Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mwigilu Nchemba amesema, “mheshimiwa spika hivi
tunavyoongea tayari ninayo hiyo ripoti ya Mkaguzi na ninaipitia mstari kwa mstari
na ninategemea baada ya bunge hili nitapitia katika maeneo hayo yanayolima
tumbaku hasa hasa mkoa wa Tabora kwa ajili ya kwenda kufuatilia utekelezaji wa
maagizo ya mheshimiwa Rais aliyoyatoa."
No comments:
Post a Comment