Na Paul Christian, Uyui.
Wakazi wa kijiji cha Ishihimulwa kata ya Bukumbi
wilaya ya Uyui mkoani Tabora wameikataa taarifa ya idara ya elimu waliyosomewa
kwenye mkutano mkuu wa kijiji hicho.
Wakazi hao wamesema idara ya elimu yenye shule ya
msingi Ishihimulwa imeeleza kuwa na mapato ya shilingi 90,000/- kwa mwaka jambo
ambalo haliendani na uhalisia wa mapato ya shule hiyo.
Akisoma taarifa hiyo ya mapato na matumizi afisa
mtendaji wa kijiji hicho Jiji Numbu amesema shule hiyo kwa mwaka ulioisha
ilikuwa na mapato hayo jambo ambalo lilipingwa vikali na wakazi hao.
Wakazi hao wameutupia lawama uongozi wa shule hiyo
ya msingi kwa kutumia vibaya na kuficha hesabu halisi ya fedha za mapato ya
shule hiyo ambayo imekodisha eneo la mnara wa kampuni ya Airtel kwa shilingi
milioni moja na laki sita kwa mwaka iweje leo mapato yawe shilingi 90,000/- kwa
mwaka.
Wamevitaja vyanzo vingine vya mapato katika shule
hiyo kuwa ni ruzuku ya shilingi 124,000/- kwa mwaka, ukodishaji wa matela ya
kukokotwa na ng’ombe ambapo tela moja ukodishwa kwa shilingi 1,000/- na wakati
huu wa masika ukodishwa kwa wastani wa mara 15 kwa siku na kipindi cha kiangazi
ni wastani wa mara 32 kwa siku.
Kutokana na hali hiyo diwani wa kata ya Bukumbi
John Majala ameiagiza kamati ya shule hiyo kuandaa na kuwasilisha hesabu za
mapato na matumizi ndani ya siku 14 ili wananchi waipate na kujiridhisha.
No comments:
Post a Comment