Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Thursday, January 28, 2016

MBOWE USO KWA USO NA WAZIRI MKUU BUNGENI DODOMA "MASWALI YA PAPO KWA PAPO"




Na Paul Christian.
FREEMAN MBOWE

Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe ameitaka serikali kutoa kauli kuhusu katazo la mikutano ya vyama vya siasa mara baada ya uchaguzi mkuu, Shirika la Utangazaji la Taifa TBC kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge na matumizi ya majeshi Zanzibar na kwingineko.

Mbowe amesema hayo leo Bungeni mjini Dodoma wakati wa kipindi cha Maswali ya papo kwa papo kwa Waziri mkuu.

Kiongozi huyo wa kambi ya upinzani Bungeni amesema, “mheshimiwa Waziri mkuu ukiwa kiongozi wa shughuli za serikali Bungeni na wewe ukiwa kama mwanasiasa mzoefu ninahakika unatambua kwamba ujenzi wa demokrasia ni gharama na mchakato wa muda mrefu na nina hakika utakuwa unajua vile vile kwamba nchi yetu imepiga hatua katika kujenga jamii inayoheshimu demokrasia, inayoheshimu sheria na inaheshimu katiba ya nchi.”

Ameongeza, “katika muda mfupi tangu serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani yapo mambo matano makubwa yaliyotokea ambayo yanahashiria aidha serikali hiyo haiheshimu kukua kwa demokrasia katika taifa ama pengine inadhamira ya kuondoa lengo kubwa hilo lililowekwa na Katiba ya taifa.”

Mbowe katika kujenga hoja ya swali lake amesema, “Mheshimiwa Waziri mkuu baada ya uchaguzi mkuu wa 2015 jeshi la polisi limeweka makatazo nchi nzima kwa vyama vya siasa kutokufanya kazi zake za siasa, haki ambayo ni ya kikatiba, na leo tayari ni miezi mitatu na siku tatu,katazo hilo linaendelea na katazo hilo mheshimiwa waziri mkuu uliliunga mkono na kusisitiza katika mkutano wako ulioufanya katika jimbo la lako la Ruhangwa kwamba wenye haki ya kufanya ni wale walioshinda lakini vyama vya siasa haviendelei kuruhusiwa kufanya kazi za siasa.”

Kiongozi huyo wa kambi ya upinzani Bungeni katika sehemu ya kwanza la swali lake ameuliza, “mheshimiwa waziri mkuu unataka kulithibitishia bunge hili,nchi hii na dunia hii kwamba wewe kama kiongozi mkuu wa shughuli za serikali unakusudio la kuendelea kuzuia vyama vya siasa kufanya shughuli zake za kisiasa ambayo ni haki yao ya Kikatiba.”

Katika sehemu ya pili ya swali lake amesema, “mheshimiwa waziri mkuu tukifuatana na hapo hapo unatambua vile vile kwamba urushaji wa matangazo ya moja kwa moja ni haki ya kikatiba ya wananchi kupata taarifa na shirika la habari la taifa ni shirika la umma, lakini ndani ya bunge mheshimiwa waziri mkuu kuna taarifa zilizorasmi kabisa serikali yako imetoa kauli hapa kuzuia urushaji huo wa matangazo.”

Mbowe ameeleza, “Sambamba na uzuiaji huo wa urushaji wa matangazo kumeendelea kuwepo kwa matumizi makubwa ya majeshi yetu, kuanzia Zanzibar hadi hapa, na Zanzibar katika kupinga matokeo ya uchaguzi ya Zanzibar ambao ulikuwa uamuzi wa wananchi, mheshimiwa waziri mkuu unaiambia nini Dunia kwa awamu yako ya Tano sasa imekubali kuwa utawala wa kijeshi kwa mgongo wa utawala wa Kidemokrasia?”

WAZIRI MKUU MAJALIWA K. MAJALIWA

Akijibu maswali hayo Waziri mkuu mheshimiwa Majaliwa Kassimu Majaliwa amesema, “Mheshimiwa Spika, kwanza niseme namshukuru sana kiongozi wa kambi ya upinzani kwa maswali yake mawili ambayo yanahitaji ufafanuzi na watanzania waweze kujua,kwamba uongozi huu wa awamu ya Tano ni uongozi unaoongoza kwa kufuata Demokrasia, kanuni, sheria na taratibu kadiri ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania ilivyo.”

Waziri mkuu ameongeza, “yapo mambo yanajitokeza na tunapojaribu kutoa maelekezo ya kimsingi kuweza kufuatilia na kwa sababu ya utaratibu wa mazoea tu yanaweza kutafsiriwa vinginevyo suala lako la makatazo ya vyama vya siasa kufanya mikutano ni jambo ambalo naweza kusema msemaji wa kwanza kabisa hakutumia nafasi yake ya uandishi kuandika kwa mfululizo kwa sababu ni mimi ndio ambaye nilikuwa nimefanya ziara kwenye jimbo langu kusalimia wapiga kura wangu.” 

Majaliwa ameendelea kujibu, “mimi ni mbunge kama nyie na ninapokuwa Ruhangwa sivai koti la waziri mkuu bali nakuwa mbunge nazungumza na watu wangu nimekuwa na vikao mbalimbali vya makundi mbalimbali nikiwashukuru binafsi kwenye jimbo langu ambako najua tunautamaduni wetu nimepita pia kwenye kata ambazo pia madiwani wetu ni wa vyama vya upinzani, lakini tumeweka msimamo wa vyama vyote kwenye jimbo lile kwamba lazima sasa tufanye kazi za maendeleo kwenye jimbo letu.”

Amefafanua, “ na kama mwandishi yule angeweza kuweka mtiririko wa ziara zangu na matamko yetu ndani ya wilaya yangu, kwa jimbo langu, angeweza kunitendea haki, kwa sababu nilichotamka mimi kilifuatiwa na kauli zilizotamkwa na madiwani kwenye kata ambako nimetembelea wakiwemo wa upinzani ambao walisisitiza na kutoa msimamo kwamba sasa jimbo hili tunataka tufanye kazi suala la siasa tunaliweka pembeni.”

Amesema, “ suala la siasa tunaondoa tofauti zetu, hayo yanazungumzwa na madiwani wenzangu wa vyama vingine kwa hiyo ni jambo jema wanapolitamka kwa wananchi wanalitamka kwa wananchi kwa maana ya kuweka msimamo wa maendeleo.”

Waziri mkuu amefafanua, “mtiririko ule tulizungumza pia na baraza la madiwani, nimezungumza na wafanyakazi wa halmashauri, nimezungumza na baraza la wazee, nimezungumza na wakinamama  na pia nikazungumza na jeshi la polisi wale ni sehemu ya raia walioko kwenye jimbo langu, mimi nimefanya kazi nyingi sana kwao na wao wamefanya kazi nyingi sana kwangu.”

Ameongeza, “Kwa hiyo kauli yangu ilikuwa inatokana na mazingira yale kama mwandishi angeamua kufanya kazi zake vizuri kwa kueleza shughuli zangu hata nilipotamka kwamba kuanzia sasa maeneo tumeamua tufanye kazi tu bila kuzingatia itikadi za vyama vyetu na kwamba sasa mambo ya siasa tuache pembeni.”

Majaliwa amefafanua, “Wale wote ambao sasa wangetakiwa kupita kwenye maeneo yawalioshinda ni wale tu ambao wameshinda kwenye maeneo yao kwa hiyo jambo lile kama lingekuwa limeelezwa, limeripotiwa kwa mtiririko ule wala lisingeweza kuleta tafsiri ambayo imekuja kutoweka.”

Amisisitiza, “mimi najua utawala wa sheria, najua vyama vya siasa vinahaki yake,najua nchi imeamua na inatambua kwamba chama cha siasa kinaweza kufanya mikutano.”

Amesema,“Lakini pia kama msingi ule wa kauli ya wanajimbo la Ruhangwa utaweza kufuatwa na watu wengine unaweza kuwaletea tija pia,kwa kusema hilo niseme tu kwamba jambo lile lilitokana na mazingira ninamoishi na sikulitamka kama waziri mkuu, nilitamka kama mbunge wa jimbo na lilitokana na matamko ya sisi wawakilishi wa vyama vya siasa tuliomo kwenye jimbo lile mheshimiwa spika.

Waziri mkuu Majaliwa akijibu sehemu ya pili ya swali aliloulizwa amesema, “eneo la pili ni lile ambalo mheshimiwa umetaka kujua kauli ya serikali juu ya TBC kuacha kutangaza siku nzima na badala yake watatangaza vipindi vya maswali na majibu baada ya hapo wataendelea na shughuli zao na huku wakirekodi ili watutangazie baadae.” 

Amesema, “mheshimiwa waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo amelifafanua vizuri sana jana kwenye kipindi maalum na ninaamini watanzania wametuelewa, haukuwa na lengo, TBC haijaacha kutangaza walichofanya ni kubadilisha ratiba, matangazo ya bunge yataendele kutangazwa lakini tumeondoa muda badala ya ule muda wao waneweza kufanya matangazo ya kibiashara na matangazo mengine.”

“Suala la bunge waandishi wao wapo, TBC inawawakilishi Dodoma watafanya rekoding halafu baadae watatafuta muda mzuri ambao tunaamini watanzania wengi watapata muda mzuri wakuweza kusikiliza matangazo yao.”Amesema Majaliwa.

 Amesema “huo ni mpango wa taasisi yenyewe wa ndani unaotokana na kazi wanazozifanya wanajua matatizo na faida wanazozipata ndani ya taasisi kwa hiyo wanapoishauri wizara, wanapoieleza wizara na kwa kuwa waliisha anza kutekeleza watanzania waliona mkatiko wa matangazo pia kulikuwa na muongozo ulitolewa hapa kwa hiyo tukasema jambo hili lazima kuwe na kauli ya serikali kwa watanzania kwa sababu muongozo ulitolewa na mmoja kati ya wabunge wetu anataka kujua kwa nini kuna mkatiko wa matangazo hivyo ndivyo ambavyo ilivyokuwa na huo nadhani msimamo wa TBC na ndio msimamo wa serikali.”

Akijibu kuhusu matumizi ya majeshi waziri mkuu amesema “Mheshimiwa ametaka pia kujua matumizi ya majeshi, majeshi  yetu yapo kwa malengo kwamba lengo kuu ni kutunza amani na utulivu ndani ya nchi,wajibu wao mkubwa ni kuhakikisha kwamba watu kwa maana ya watanzania kwa majeshi ya Tanzania wajibu wake ni kuhakikisha watu wetu wanafanya shughuli zao kwa amani na utulivu na wako nchi nzima.

Ameongeza kusema, “jukumu lao ni kumlinda mtanzania popote alipo bila ya kukiuka misingi ya jambo analolifanya wakati huo, wako pia Zanzibar, wako pia Tanzania Bara na wote hao kazi yao na jukumu lao ni lile lile sasa wanaweza kulazimika kutumia nguvu pale ambako wanapoona utaratibu ulioko eneo hilo unakiukwa.”

Majaliwa amesisitiza, “ na hiyo ndio kazi ya jeshi na polisi kwamba wataendelea kutunza amani ili watanzania walioko kwenye eneo hilo kila mmoja afanye shughuli yake kila mahali kunautaratibu wake, kila mahali kuna msingi wake na ningetarajia eneo hilo, wote walioko kwenye eneo hilo, wanaofanya jambo hilo, wafanye jambo hilo kwa msingi unaofanana, usiokiuka taratibu za eneo hilo kwa hiyo jeshi la polisi lipo na litaendelea kufanya kazi yake kwa uaminifu, uadilifu na ninaomba sana tuwasaidie jeshi la polisi kufanya kazi yao bila ya usumbufu ili wasionekane wanafanya kazi nje ya utaratibu wao.”

      
  


No comments: