Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Wednesday, July 27, 2016

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO



Na Paul Christian, Tabora.

Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu katika kupanga na kutumia rasilimali watu na fedha katika kujiletea maendeleo.

Diwani wa kata ya Cheyo katika manispaa ya Tabora Yusuph Kitumbo ameyasema hayo wakati wa mahojiano maalum kuhusu utekelezaji wa ahadi na ilani ya Chama Cha Mapinduzi katani humo.

Amesema, “kimsingi matumizi bora ya rasilimali watu,fedha na wakati yanategemea mawasiliano madhubuti baina ya viongozi wa ngazi za mitaa na wananchi wanaowaongoza ambapo uibua na kupanga vipaumbele vya maendeleo.”

Kitumbo amesema alianza rasmi kazi ya udiwani mwezi wa Disemba mwaka jana ambapo kazi yake ya kwanza ilikuwa ni kutengeneza daraja la mawasiliano kati ya viongozi na wananchi wa kata hiyo.

Amefafanua kuwa jambo hilo limefanikiwa kwa kuwa katika kipindi cha miezi minane tu ameweza kuongeza watendaji wa mitaa wanne kutoka wawili waliokuwepo kabla ya uchaguzi.

Diwani huyo amesema watendaji hao kwa kushirikiana na wenyeviti wa mitaa wameweza kutengeza mnyororo wa mawasiliano katika kuzikabili kero na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye mitaa yao.

Amesema, “kutokana na hali hiyo kata ya cheyo kupitia kamati ya maendeleo  imeweza kuibua mipango ya vipaumbele katika sekta za elimu,afya, miundombinu ya barabara, kusaidia wenye uhitaji watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu,wazee na makundi ya ujasiria mali.”

Kitumbo amebainisha kuwa wameweza kutumia fedha zao kuchonga barabara za mitaa ambazo hazikuwepo na kuifanya kata hiyo ambayo ni makazi ya viongozi wa serikali ngazi ya mkoa na wilaya kutofikika kwa urahisi kwenye baadhi ya maeneo.

“Katika kipindi hiki angalau tumetatua kero ya barabara ambazo hazikuwepo na kuifanya kata yangu kufikika kwa urahisi kwa zaidi ya asilimia 50.”Amesema diwani huyo.

Ameongeza kuwa licha ya kuzichonga barabara hizo bado zitakabiliwa na changamoto ya kusombwa au kujaa maji wakati wa mvua hivyo anapigania kupata barabara za lami ili kuwe na uhakika wa kupitika majira yote.

Diwani huyo wa kata ya Cheyo amesema katika suala la kuhakikisha kila mwanafunzi anakaa juu ya dawati, kata yake imeweka rekodi ya kuondoa upungufu wa madawati mapema zaidi kuliko kata nyingine katika manispaa hiyo.

Kitumbo amebainisha kuwa kata ya Cheyo ilikuwa kata pekee kati ya kata 29 ya Manispaa hiyo kupokea madawati 50 kutoka kampuni ya mawasilino ya TIGO jambo lililoondoa upungufu uliokuwepo.

Amesema, “Ingawa kumekuwa na ongezeko kubwa  la wanafunzi wanaoandikishwa katika shule za msingi sita kwenye kata yetu, vyumba vya madarasa vinatosheleza mahitaji.”

Diwani huyo amefafanua kuwa shule hizo za msingi zilikuwa na changamoto ya kugharamia mishahara ya walinzi, ulipaji wa Ankara za maji na umeme ambalo nalo limepatiwa ufumbuzi kwa sasa.

“Kwa sasa shule ya msingi Cheyo A inakabiliwa na changamoto ya madarasa matatu kujaa maji wakati wa mvua kutokana na  ujenzi wa barabara ya kilimatinde,jambo ambalo tunalitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na wahandisi wa Manispaa na TANROADS.”ameongeza Kitumbo.

Kwa upande wa shule ya sekondari ya Cheyo, amesema licha ya kufanya vizuri inakabiliwa na upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
Katika kukabiliana na hali hiyo, amesema, “mimi mwenyewe nimejitolea kuwafundisha wanafunzi wa shule hiyo masomo ya Hisabati,Fizikia na Kemia ili nitoe mchango wangu kipindi hiki kigumu.”

Kitumbo amebainisha kuwa katika shule hiyo ya sekondari wamepata mradi wa ujenzi wa vyumba vine vya madarasa na matundu 16 ya vyoo kwa uwiano wa matundu manane kwa ajili ya wavulana na mengine manane kwa ajili ya wasichana.

Aidha amesema mradi huo wa ujenzi utagharimu kiasi cha shilingi milioni 132, fedha ambazo ziko kwenye akaunti ya shule na kwamba ujenzi huo unasimamiwa na Bodi ya shule hiyo.

Kitumbo amesisitiza kuwa fedha hizo zitasimamiwa kwa umakini ili kuhakikisha zinatumika kwa lengo lililokusudiwa na ikibidi zifanye jambo lingine kwa manufaa ya shule hiyo.

Diwani wa kata hiyo ameanisha mipango ya muda wa kati ni kuwasaidia watu wenye mahitaji wakiwemo wazee, wenye ulemavu,watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira hatarishi  ili waweze kupata huduma muhimu za kijamii.

Amezitaja  licha ya serikali kutoa elimu bure bado watoto hao wanahitaji chakula,mavazi na malazi ambapo kwa upande wa wazee ni kuhakikisha wanapata huduma za afya bure.

Kwa upande wa Afya amebainisha kuwa katika zahati ya Cheyo ilikuwa ikikabiliwa na upungufu wa watumishi, huduma duni na ukosefu wa dawa pamoja na vifaa tiba.

“Lakini kwa sasa Zahanati ile ni moja kati ya zahanati zinazotoa huduma nzuri za afya, kwa kuwa inawatumishi wa kutosha, dawa zinapatikana pamoja na huduma zimeboreka zaidi.” Amesema.

Akizungumzia malengo mengine ya muda wa kati na mrefu, Kitumbo amesema ni kujenga kituo cha Polisi, Soko na kuipandisha hadhi zahanati iliyopo sasa kuwa kituo cha afya.

No comments: