![]() |
PAROKIA YA KANISA KATOLIKI ULYANKULU |
Na Paul Christian, Ulyankulu.
Mtemi Milambo
aliyeishi zaidi ya miaka 132 iliyopita anaelezwa kuwa miongoni mwa waafrika
wachachewa wakati huo walitumia choo.
Akizungumzia mambo ya
kihistoria yaliyopo hivi sasa katika tarafa ya Ulyankulu wilaya ya Kaliua
mkoani Tabora diwani wa kata ya Uyowa Alphonce Msanzya amesema hadi leo hii
shimo pamoja na miti iliyokuwa ikitumiwa kwenye choo hicho vipo.
Diwani huyo ameeleza
kuwa hali hiyo inamaanisha mtemi Milambo alikuwa mtu aliyestaarabika na upeo
mkubwa wa kutambua na kufahamu mambo mbalimbali ya mahusiano, utawala,ulinzi na
matumizi ya zana bora.
Msanzya amesema, “katika
kitongoji cha Itambilo, kijiji cha Songambele kata ya Uyowa kuna mti aina ya “Mhama”
ambao ulitumiwa na askari wa mtemi Milambo waliojulikana kama “walugaluga” kwa
ajili ya kufanya mazoezi ya kulenga shabaha kwa kutumia bunduki.”
Diwani huyo anafafanua
kuwa mti huo hadi leo upo katika eneo hilo na unazo alama za matundu ya risasi
na hivyo kudhihirisha kuwa mtemi huyo alitumia zana mbalimbali kutoka nje ya
eneo lake la kiutawala.
Amesema jambo lingine
la kihistoria lililopo kwenye tarafa hiyo ni katika eneo la barabara ya kutoka
Ulyankulu kuelekea Kahama maarufu kama barabara ya sita ambapo limewekwa
karavati.
Msanzya amebainisha
kuwa karavati hilo limewekwa hapo kutokana na kuwepo kwa handaki lililochimbwa na
askari wa mtemi Milambo “walugaluga” wakati akijiandaa kumshambulia mjomba
wake.
Amefafanua kuwa lengo
la mtemi Milambo lilikuwa ni kuyafikia makazi ya mjomba wake kwa kupitia
handaki na kisha kumshambulia lakini kitendo hicho hakikumfurahisha mama yake
mzazi Milambo ambaye kwa wakati huo
alikuwa akiishi kwa kaka yake ambaye ndiye huyo mjomba wake na mtemi Milambo.
Msanzya ameeleza kuwa
wazee wa maeneo hayo wanasema kuwa mtemi Milambo alifanikiwa kuchimba handaki
hilo na kuyakaribia makazi ya mjomba wake kwa lengo la kufanya shambulio.
“Lakini siku moja akiwa
kwenye harakati hizo mtemi Milambo aliletewa ugali ambao inasemekana kwa
mazingara ulibadilishwa na kupewa ugali wenye sumu ambapo aliula na kuanza
kuugua kwenye mfumo wa chakula kuanzia mdomoni, kwenye koo hadi tumboni.
Msanzya amesema na
hiyo ndio sababu Padri mmoja aliwahi kuandika kuwa mtemi Milambo alikufa kwa
kansa ya koo.
Diwani huyo ametaja
eneo linguine lilibaki na kumbukumbu ya kihistoria ni eneo ambalo Parokia ya
kanisa Katoliki Ulyankulu limejengwa kwa kuwa lilikuwa ni ngome ya ikulu ya
mtemi Milambo.
![]() |
ENEO LILILOCHIMBWA HANDAKI |
Amesema kitu kingine cha kusisimua katika eneo hilo ni kaburi la mtemi Milambo lililopo kwenye kitongoji cha Ikonongo ambapo pia kuna kifusi kikubwa cha nyumba aliyokuwa akiishi mtemi huyo mashuhuri.
Msanzya amebainisha
kuwa katika eneo hilo kuna makaburi ya
watemi waliotawala kabla na baada ya mtemi Milambo.
Amesema hata kiti
alichokuwa akikitumia mtemi Milambo wakati wa shughuli zake mbalimbali zikiwemo
za kiutawala ukifika huko utakikuta hadi leo kipo.
Diwani huyo wa kata ya
Uyowa amesema kwa ujumla mkoa wa Tabora umejaliwa kuwa na historia ya kipekee
jambo muhimu linalopaswa kufanywa ni kuutangaza utajiri wa kihistoria uliopo
ili uanze kuwanufaisha watu wetu.
No comments:
Post a Comment