Na Saida Issa, Tabora.
Zahanati ya kijiji cha Ikomwa katika Manispaa ya
Tabora inakabiliwa na upungufu mkubwa wa dawa na vifaa tiba hali inayasabisha
usumbufu kwa wakazi wanaohudumiwa na zahanati hiyo.
Hayo yamebainishwa na wakazi hao mbele ya diwani
wa kata hiyo mheshimiwa Salum Msamazi Lugembe wakati wa ziara ya kutembelea
kijiji hicho kwa lengo la kusikiliza kero za wakazi hao.
Hamad Shaban mkazi wa kijiji hicho amesema ukosefu
wa vifaa vya kupimia kunawafanya watumishi wa afya kuwapima kwa macho na
maelezo ya mgonjwa na kisha kuwapa dawa ya malaria aina ya Mseto hali
inayohatarisha afya zao.
Mkazi huyo pia amesema zahanati hiyo inawahudumu
wachache wasiokidhi mahitaji ya wagonjwa wanaofika kuhudumiwa.
Mkazi wa Kijiji cha Kapunze katika kata hiyo Amina
Juma amebainisha kuwa ukosefu wa barabara ya uhakika inayounganisha kijiji
hicho na zahanati kumewasabisha kushindwa kufika kwenye zahanati kufuatia
kufunikwa na maji katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha.
Amesema hali hiyo inawaathiri sana akinamama
wajawazito na watoto wadogo kwa kuwa hawana njia mbadala ya kufikia huduma ya
afya na hasa wakati wa dharura.
Akijibu hoja hizo za wananchi diwani wa kata hiyo
Salum Msamazi Lugembe amesema kero ya barabara inayounganisha kijiji cha
Kapunze na Ikomwa ataifikisha mbele ya kikao cha baraza la madiwani ili
itengewe bajeti na kutengenezwa.
Diwani huyo ameanza ziara ya siku mbili ambapo
anasikiliza kero za wananchi katika vijiji na kutembelea taasisi zilizopo katani humo kabla ya kuanza vikao vya
baraza la madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Tabora .
No comments:
Post a Comment