Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, January 2, 2016

SEHEMU YA KWANZA:TUNAJIFUNZA NINI KWA TUKIO HILI LA KIHISTORIA



                                      OPERESHENI ENTEBBE


Paul Christian, Tabora.

Ilikuwa majira ya saa tano usiku wa tarehe 3 Julai 1976 makomandoo wapatao 100 wa jeshi la Israel (IDF) walivamia uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Entebbe nchini Uganda na kuwakomboa mateka wenye asili ya Israel waliokuwa wakishikiliwa kwenye moja ya majengo ya uwanja huo.

Uvamizi huo wa  jeshi la Israel ulipewa jina la  Operesheni Entebbe au Thunderbolt au Yonatan “Jonathan” kwa kumbukumbu ya luten Kanali Yonatan Netanyahu askari pekee wa Isarel aliyeuawa kwenye operation hiyo.

Wiki moja kabla ya operesheni hiyo tarehe 27 Juni, 1976 ndege ya abiria Air  France 139, aina ya  Airbus A300B4-203, yenye namba za usajili F-BVGG (c/n 019),  ilikuwa ikisafiri kutoka Ben Gurion,Israel kuelekea Charles De Gaulle,Ufaransa kupitia Ellinikon,Ugiriki ilitekwa nyara. 

Ndege hiyo ilikuwa na abiria 248 na wafanyakazi 12 ilitekwa nyara na wapiganaji wa kundi la ukombozi wa wapalestina yaani  Popular Front for the Liberation of Palestine – External Operations (PFLP-EO)  kwa amri ya  kiongozi wa kundi hilo Wadie Haddad

Kundi hilo la PFLP-OE lilijitenga kutoka  kundi mama la Popula Front for the Liberation of Palestine PFLP lililokuwa likiongozwa na George Habash.

Ndege hiyo ilitekwa Nyara na wapiganaji hao baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa Ellinikon  jijini Athens, Ugiriki ambapo abiria 58 wakiwemo wateka nyara wanne walipanda.

Mara baada ya kuondoka kwenye uwanja huo wateka nyara hao waliibuka na kuwataka marubani kuiongoza ndege hiyo kuelekea Benghazi Nchini Libya ambapo ilikaa kwa saa saba kwa ajili ya kuongeza mafuta.

 Ndege hiyo ikiwa Benghazi,  watekaji hao walimwachia huru mateka mmoja mzaliwa wa uingereza mwenye uraia wa Israel Patricia Martell ambaye alijifanya ameharibu ujauzito wake kwa mshituko.
 
Hatimaye Ndege hiyo ya Air France 139 iliondoka Benghazi na kutua  kwenye uwanja wa ndege wa kimaitaifa wa Entebbe nchini Uganda majira ya saa 9 na dakika 15 Alasiri siku ya tarehe 28 Juni, 1976. 

Rais wa Uganda Idd Amin binafsi aliwaunga mkono watekaji hao na kuwakaribisha kwenye ardhi ya Uganda.Aliwatembelea mara kwa mara na kuwaambia mateka hatua za mazungumzo ili waachiwe huru.

Mnamo tarehe 28 Juni, 1976  Wateka Nyara hao wanne ambao wawili wakiwa wapalestina na wengine wawili wakiwa wajerumani wanachama wa kundi la German Revolutinary Cells, walitoa madai yao kwa serikali ya Israel.

Katika madai yao watekaji hao walitaka kuachiliwa huru wafungwa 40 wakiwemo wanamgambo wa kipalestina waliofungwa kwenye magereza ya nchini Israel.

Pili, walitaka kuachiwa huru kwa wafungwa wengine 13 waliofungwa kwenye magereza ya mataifa mengine manne.

Tatu,walitaka kulipwa kiasi cha dola za kimarekani milioni 5 kwa ajili ya kuiachia huru ndege hiyo ya Air France 139 na kwamba madai hayo yalipaswa kutekelezwa hadi kufikia tarehe 1 Julai, 1976. 

Ndege hiyo ilipotua kwenye uwanja huo wa Entebbe huku ikilindwa na askari wa jeshi la Uganda, abiria pamoja na wafanyakazi wote wa ndege hiyo waliamriwa kushuka na kisha kupelekwa kwenye jengo la zamani lisilotumiwa kwa shughuli za abiria.

Mnamo tarehe 29 Juni, 1976 abiria mateka walitengwa makundi mawili baada ya jeshi la Uganda UDF kubomoa ukuta uliokuwa ukiwatenganisha chumba cha mapokezi na chumba kingine katika jengo hilo.

Watekaji waliwachambua na kuwatenga raia wa Israel wakiwemo raia wa Israel wenye uraia wa nchi mbili kutoka kwa raia wa nchi nyingine miongoni mwa mateka hao, na raia hao wa Israel waliamriwa kuingia kwenye chumba kimoja. 

Aidha mateka wasio kuwa raia wa Israel waumini wa madhehebu ya Orthodox wanandoa wanne kutoka Marekani na Ubelgiji, na Mfaransa mkazi wa Israel waliunganishwa kwenye kundi lililotengwa la waisrael.

Kwa mujibu wa aliyekuwa mmoja wa mateka hao watano mfaransa Monique Epstein Khalepski alisema walichukuliwa na watekaji kwa ajili ya mahojiano kwa kuwahofiwa kuficha utambulisho wa uraia wao.

Naye Mateka Mfaransa Michel Cojot-Goldberg alisema watekaji walishindwa kumtambua muisrael mateka aliyekuwa afisa wa jeshi mwenye uraia wa nchi mbili baada ya kuonesha paspoti isiyokuwa ya Israel na baadae aliondoka na kundi la pili la mateka walioachiwa huru.

Raia wa Marekani Janet Almog, Mwanamke Mfaransa Jocelyne Monier ambaye mwenzi wake alikuwa muisrael, na Jean-Jacques Mimouni mwenye uraia wa nchi za Ufaransa na Israel ambaye jina lake halikuitwa kwenye orodha ya majina ya abiria, walichagua kwa hiari zao kujiunga na kundi la mateka wa Israel.

Tarehe 30 Juni, 1976  watekaji waliwaachia huru mateka 48 kutoka kwenye kundi la mateka wasiokuwa raia wa Waisrael ambao wengi wao walikuwa wazee, wagonjwa, wakinamama na watoto. 

Mateka 47 kati yao walisafirishwa kueleka Paris, Ufaransa, na abiria mmoja Dora Bloch mwenye umri wa miaka 75 alipelekwa hospitali nchini Uganda kutokana na hali yake ya afya kuwa mbaya.

Tarehe 1 Julai, 1976 ilikuwa siku ya mwisho iliyotolewa na watekaji hao ili madai yao yatekelezwe, serikali ya Israel ilikubali kufanya mazungumzo kuhusu madai ya watekaji.

Kutokana hali hiyo watekaji wakaongeza siku za mazungumzo na kwamba siku ya mwisho ya utekelezaji wa madai yao ikawa majira ya mchana ya tarehe 4 Julai, 1976.

No comments: