![]() |
MKUU WA WILAYA YA TABORA SULEIMAN KUMCHAYA AKIWAHUTUBIA MADIWANI WA HALMASHAURI YA MANISPAA YA TABORA WAKATI WA UFUNGUZI WA SEMINA YA UPATIKANAJI WA MAJI KATIKA MANISPAA HIYO |
Na Paul Christian, Tabora.
Madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Tabora
wameagizwa kuongoza mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira katika maeneo ili
kulinda uoto wa asili unaosababisha maji, mvua, rutuba na kuongeza mazao ya
chakula na biashara.
Agizo hilo limetolewa leo na mkuu wa wilaya ya
Tabora Suleiman Kumchaya wakati akifungua semina ya siku moja iliyohusu hali ya
upatikanaji wa maji katika manispaa hiyo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maji Safi
na Usafi wa Mazingira TUWASA na
kufanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mamlaka hiyo.
Amesema wananchi wanahatarisha vyanzo vya maji kwa kukata miti, kuchungia
mifugo na hata kufyeka misitu kwa shughuli za ufugaji,biashara kilimo, na makazi
hali inayopaswa kupigwa vita kwa nguvu
zote.
Kumchaya amebainisha kuwa bwawa la Igombe
linalotegemewa kama chanzo cha maji kwa wakazi wa mji wa Tabora liko kwenye
hatari ya kukauka endapo viongozi na wananchi hawatachukua hatua za makusudi
kulinda mazingira ya vyanzo vya maji.
Aidha mkuu huyo wa wilaya amewanyooshea kidole
wanasiasa kuacha tabia ya kuwatetea wananchi wanaovamia maeneo yaliyotengwa au
kuharibu mazingira kwa makusudi kwa madai ya kuwa wahusika ni wapiga kura wao.
Kumchaya amewataka madiwani hao kutumia kamati zao
za maendeleo ya kata kujadili na kupanga mambo ya maendeleo ikiwemo kulinda
na kuhifadhi mazingira katika maeneo yao.
Amewasisitiza madiwani hao kuwa na ratiba endelevu
ya kutembelea, kusimamia,kukagua na kuwaelimisha wananchi wao juu ya umuhimu wa
kutunza mazingira.
Mkuu huyo wa wilaya amesema athari za uharibifu wa
mazingira katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Tabora zimeanza kuonekana
kutokana na mvua kupungua ukilinganisha na miaka ya nyuma.
No comments:
Post a Comment