Na Paul Christian, Ulyankulu.
Halmashauri za serikali za vijiji katika jimbo la
Ulyankulu wilaya Kaliua mkoani Tabora wameagizwa kuwa na orodha ya wakazi (rejista)
katika maeneo yao ili kuwatambua wageni wanaoingia kwenye vijiji hivyo.
Agizo hilo limetolewa na afisa tarafa wa Ulyankulu
John Chitanda alipokuwa akizungumza kwenye kikao kilichowakutanisha wenyeviti
wa vitongoji na vijiji, maofisa ugani, watumishi wa afya,walimu wakuu na wakuu
wa shule katika ukumbi wa mikutano wa kanisa katoliki barabara ya 13.
Amesema orodha ya wakazi katika vijiji itasaidia
kuwatambua wageni na hivyo kudhibiti uhalifu, uingizaji wa mifugo, uhifadhi wa
mazingira na upangaji wa matumizi bora ya ardhi.
Chitanda amebainisha kuwa utaratibu huo ulikuwepo
huko nyuma na ulisaidia kuwatambua wageni na hivyo kudhibiti uhalifu katika
vijiji hivyo.
Afisa tarafa huyo amesema tarafa ya Ulyankulu
inapakana na hifadhi za mapori ya akiba ambayo yamekuwa yakivamiwa na mifugo
inayotoka nje ya tarafa hiyo huku viongozi wa serikali za vijiji wakidai hawana
taarifa kuhusu wamiliki wa mifugo hiyo.
Chitanda amesema kitendo hicho huenda kinafanywa
kwa makusudi na viongozi hao kwa kuwa wanapokea rushwa kutoka kwa wafugaji ili
waingize mifugo ambayo inazidi uwezo wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya
marisho na maji jambo linalosababisha waingie kwenye maeneo ya hifadhi.
Amewashauri viongozi wa serikali za vijiji kutojiamulia
kupokea mifugo pasipo kuhusisha wananchi kupitia mikutano mikuu ya vijiji
kulingana na uwezo wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili hiyo ili kuepusha migogoro
baina ya wafugaji na wakulima au wafugaji na maofisa wa uhifadhi wa mapori ya
akiba.
Aidha afisa tarafa huyo amehimiza kufanya ziara ya
kushitukiza kukagua rejista hiyo ya wakazi na namna inavyotumika kuorodhesha wakazi
wote waliopo kwenye vijiji na watakao bainika kutotekeleza agizo hilo
watachukuliwa hatua za kinidhamu.
No comments:
Post a Comment