Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Tuesday, January 26, 2016

WAKUU WA IDARA NA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA SIKONGE WATAKIWA KUWEKA NAMBA ZA SIMU HADHARANI



Na Allan Ntana, Sikonge

Wakuu wa idara na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora wameagizwa kuweka namba zao za simu za kiganjani hadharani ili kupambana na urasimu wa huduma kwa wananchi unaofanywa na baadhi ya watendaji au wataalamu wa halmashauri hiyo.

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Peter Nzalalila katika kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika jana mjini Sikonge.

Amesema baadhi ya watumishi wa umma hawatoi huduma inayostahili kwa wateja wao badala yake wamekuwa wakiwanyanyasa na kwa kauli za njoo kesho, mhusika hayupo au kutoa lugha zisizofaa kwa wananchi jambo ambalo ni kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma.

‘Kila aliyepewa dhamana ya kutumikia wananchi katika idara yoyote ile
ya serikali anapaswa kufuata maadili ya kazi yake na ya utumishi wa
umma kwa kumhudumia mteja wake ipasavyo pindi anapoenda kwake kupata huduma, na si vinginevyo.” Amesema Nzalalila

Amesema, ‘Kuanzia sasa ili kudhibiti vitendo vya unyanyasaji wananchi
vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu,
viongozi wote tunapaswa kuweka namba zetu za simu hadharani ili wananchi watupe taarifa za vitendo hivyo.”

Mwenyekiti huyo wa halmashauri amewataka  wananchi wa wilaya hiyo kuwapa ushirikiano viongozi wao kwa kutoa taarifa za vitendo vyovyote vya uonevu au unyanyasaji vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa umma wasio waadilifu ili hatua kali za kinidhamu ziweze kuchukuliwa dhidi ya watumishi wa aina hiyo.

Amesisitiza kutotaka kuona watumishi wa halmashauri hiyo wakifanya kazi kwa mazoea katika kipindi cha Uenyekiti wake na amewataka kutekeleza majukumu yao ipasavyo chini ya kauli mbiu hapa kazi tu.

Mkuu wa wilaya hiyo Hanifa Selengu alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri hiyo Philemon Magesa kugawa mwongozo wa mgawanyo wa fedha za serikali za kugharamia elimu bure katika wilaya hiyo ili
kuwarahisishia ufutaliaji wake.

Ili kuhakikisha zinatumika ipasavyo Selengu aliwataka watumishi wa
halmashauri hiyo na madiwani wote kufuatilia fedha hizo kwa umakini
mkubwa na kujua matumizi yake jambo ambalo liliungwa mkono na
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo.

No comments: