Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Wednesday, January 20, 2016

DOKTA KITAPONDYA:UJUE UGONJWA WA U.T.I



 
DOKTA DEUS KITAPONDYA

Na Paul Christian, Tabora.

Dokta Deus Kitapondya wa EFATHA Dispensary mjini Tabora amesema ugongwa wa U.T.I ni ugonjwa unaoathiri njia ya mkojo na zaidi huwashambulia wanawake kutokana na sababu za kimaumbile.

Amesema U.T.I ni kifupi cha Urinary Track  Infection ni ugonjwa ambao unawaathiri pia watoto wadogo.

Amesema ugonjwa huo uathiri mfumo wa mkojo ikiwa ni pamoja na mirija ya mkojo kutoka kwenye figo (ureter), kibofu cha mkojo na mrija kwa kupitisha mkojo kutoka kwenye kibofu na kisha  kutoka nje ya mwili (urethra).

Dokta Kitapondya amebainisha kuwa ugonjwa huo pia unaweza kuathiri figo kama hakudhibitiwa mapema.

Amesema ugonjwa huo husababishwa na bakteria anayeitwa Escherichia coli (E. coli) ambao kwa sehemu kubwa makazi yao  ya kawaida ni kwenye utumbo mpana, na hivyo huwa wanapatikana pia kwenye haja kubwa.

Aidha amesema bakteria hao wa Escherichia coli hawasababishi peke yao U.T.I bali huambatana na wengine waitwao staphylococcus, saprophyti cus, pseudom onas, enterobacter na kadhalika.

Dokta Kitapondya ameeleza kuwa U.T.I inaambukizwa kwa kutumia vyoo vichafu kwa kuwa ndani ya vyoo kunabakteria wengi,kutumia maji machafu wakati wa kujisafisha au kuoga, unywaji wa vinywaji vyenye sukari kwa muda mrefu pamoja na kutokunywa maji ya kutosha.

Amezitaja sababu nyingine kuwa ni upungufu wa homoni ya wanawake iitwayo Oestrogen husababisha bakteria wanaosababisha maambukizi katika njia ya mkojo kuzaliana kirahisi.

Mtaalam huyo wa afya ametaja kufanya ngono na mtu mwenye bacteria wa U.T.I unaweza kuambukizwa.

Dokta Kitapondya amezitaja baadhi ya dalili za mtu aliyeambukizwa  U.T.I  kuwa ni maumivu wakati wa kukojoa, mkojo kuwa na rangi ya njano kupindukia na kuwa na harufu kali ijapokuwa siyo kila mwenye dalili hizo ana maambukizi katika njia ya mkojo.

Dalili nyingine za U.T.I ni  kutokwa na usaha wakati wa kukojoa, kabla au baada ya kukojoa ukiambatana na maumivu na kuhisi moto wakati mkojo ukitoka.

Amesema baadhi ya watu wenye U.T.I hupata vichomi katika njia ya mkojo, kuhisi kuwashwa sehemu za siri, kuumwa kiuno au tumbo na kadhalika.

Dokta Kitapondya ameeleza mgonjwa wa U.T.I anaweza pia kukumbwa na homa kali ya mara kwa mara,mwili kuwa mchovu na kwa watoto hupoteza hamu ya kula na mwili huonesha kuchoka.

Amesema wagonjwa wengine hupata maumivu kwenye kibofu cha mkojo ambapo husikia maumivu ya chini ya tumbo usawa wa kitovu yasiyoisha.

Hata hivyo amesema U.T.I  hutibika kwa dawa mbalimbali za kisasa baada ya kufanyiwa vipimo na kuthibitika kuwa mgonjwa ana maambukizi hayo.

Dokta Kitapondya amesisitiza kuzingatia usafi kwa kujisafisha kwa kutumia maji yaliyosalama, kufanya ngono salama na kuwaona wataalam wa afya mara unapohisi maambukizi kwenye mfumo wa mkojo.

No comments: