Na Paul Christian, Tabora
Halmashauri ya Manispaa na wilaya mkoani Tabora
zimeshauriwa kuwekeza kwenye miradi ya
kuvuna maji ya mvua ikiwa ni pamoja na kuchimba mabwawa yatakayo tumika kwa
kilimo cha umwagiliaji ambacho kitazalisha ajira kwa vijana na akinamama.
Ushauri huo umetolewa na katibu wa siasa, itikadi
na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Uyui Said Katala alipofanya
mahojiano maalum na Tabora Watch kuhusu mbinu za kukabiliana na tatizo la ajira
mkoani Tabora.
Amesema endapo halmashauri zitaibua miradi ya
kuchimba mabwawa, kujenga mabanio ya kukinga maji na mifereji katika maeneo ya
mabonde itasaidia kuinua shughuli za kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Katala amesema kuibua, kusimamia na kuendeleza
miradi kama hiyo katika kilimo itasaidia kutoa ajira kwa watu wengi kwa wakati
mmoja.
Aidha ameeleza kuwa wakazi wa maeneo mengi katika
mkoa wa Tabora huwa wanakumbwa na njaa
mara kwa mara na ili kukabiliana na tatizo hilo halmashauri ziwekeze kwenye
kilimo cha umwagiliaji.
![]() |
SAID KATALA |
Katala amesema wakati umefika kwa wataalam kutumia
elimu zao kuisaidia jamii kuondokana na umasikini, ukosefu wa ajira na baa la
njaa kwa kuwekeza katika uvunaji wa maji ya mvua.
Katibu huyo muenezi amesema katika msimu huu wa
mvua sehemu kubwa ya mkoa wa Tabora imepata mvua nyingi ambayo maji yake
yanapotea bure na wakati mwingine kuleta madhara kwenye mashamba na makazi ya
wananchi.
Amesema uvunaji wa maji hayo ni jambo linalopaswa
kuangaliwa kwa umakini wa kipekee kwa lengo la kukuza uchumi wa mkoa wa Tabora.
No comments:
Post a Comment