Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, January 2, 2016

KUMCHAYA:MKAPA NI KIOO CHA WAANDISHI WA HABARI KUONGEZA MAARIFA NA UFAHAMU



Rais wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa

Na Paul Christian, Tabora.

Waandishi wa habari mkoani Tabora wameaswa kuongeza maarifa na ufahamu kwa kusoma vitabu na machapisho mbalimbali ili kuongeza tija katika kazi zao za kuhabarisha, kujulisha na kuburudisha.

Mkuu wa wilaya ya Tabora Suleiman Kumchaya amesema hayo alipokua akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake katika kuutathimini mwaka 2016 na tasnia hiyo.

Amesema, “Kusoma sana kunaongeza uwezo wa kufahamu na kuchambua mambo mbalimbali kwa kina, hali hii itawafanya waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi kuliko ilivyosasa.”

Mkuu huyo wa wilaya amehimiza waandishi hao kutopuuza suala la kusoma kwa kuwa mwaka 2016 utakuwa wa mabadiliko katika Nyanja za kiuchumi,kisiasa,kijamii na kiutamaduni na kwamba uchambuzi yakinifu wa waandishi hao utasaidia kuharakisha mabadiliko hayo.

Kumchaya amewataka waandishi hao kuiga mfano wa Rais wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa ambaye muda wake mwingi anautumia kusoma vitabu na machapisho mbalimbali hata wakati akiwa Rais wa nchi.

“Mzee Mkapa akiwa kiongozi wa nchi hakupenda vitu vya anasa hata anapokuwa nje ya nchi muda mwingi aliutumia kusoma vitabu.” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Kumchaya ambaye aliwahi kuwa msaidizi wa Rais huyo wa awamu ya tatu amesema, “ukitaka kuelewana na mzee Mkapa mwambie nimeona kitabu kizuri mahali fulani na sio viatu vizuri au vitu vya anasa.”

Suleiman Kumchaya amewahi kufanyakazi kwenye shirika la utangazaji Tanzania TBC zamani likijulikana kama Radio Tanzania na idhaa zake mbalimbali.
Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa ni mwandishi wa habari na amewahi kuwa mwandishi wa Rais wa awamu ya kwanza Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

No comments: