Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Sunday, January 31, 2016

POLISI TABORA YAFIKISHA POINTI 24 BAADA YA KUWACHEZESHEA KICHAPO CHA KI-FFU, GEITA GOLD MINE


Na Ramadhan Faraji, Tabora.

Ligi daraja la kwanza imeendelea kushika kasi Jumapili  kufuatia timu ya Polisi Tabora kuikaribisha timu ya Geita Gold Mine kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa iliwasisimua mashabiki wa Polisi Tabora ambao walikuwa na shahuku ya kuiona timu yao ya nyumbani ikifanikiwa kuondoka na pointi 3 muhimu na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kupanda ligi kuu ya Tanzania Bara.

Iliwachukua dakika 81 Polisi Tabora kupitia kwa mchezaji wao Ked Mohamed kuwanyanyua mashabiki wao baada ya kupachika bao la kwanza na la ushindi.

Kwa ushindi huo Polisi Tabora imefikisha pointi 24 sawa na wapinzani wao Geita Gold Mine ambao wanaongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 24 na wakiwa na tofauti ya goli moja.

Polisi Tabora ambayo inanyemelea nafasi ya kucheza ligi kuu Tanzania Bara pamoja na wapinzani wao Geita Gold Mine wamebakiza mechi mbili kila timu ili kukamilisha mzunguko wa pili wa ligi daraja la kwanza ambao utaamua timu ipi ipande daraja.

Mwishoni mwa wiki hii Polisi Tabora watawafuata maafande JKT Kanembwa huko Kigoma wakati Geita Gold Mine watawafuata maafande wa JKT Oljoro mjini Arusha.

Tabora Watch inawatakia kila la heri Polisi Tabora kwenye mbio hizo za kupanda daraja.

Wakati huo huo siku ya Jumamosi Rhino Rangers ya Tabora ikiwa kwenye uwanja wa ugenini mjini Musoma ilipoteza mechi yake mbele ya maafande wa Polisi Mara baada ya kukubali kichapo cha bao1 kwa 0 ikiwa ni mwendelezo wa ligi daraja la Kwanza.



No comments: