Na lucas Raphael,Igunga.
Wakulima wa zao la mpunga katika skim
ya Umwagiliaji Mwamapuli wilayani Igunga mkoani Tabora wametakiwa kuachana na
kilimo cha mazoea na badala yake wawe na mpango kazi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya
ya Igunga Ziporra Pangani baada
ya kituo cha utafiti wa kilimo cha Tumbi katika manispaa ya Tabora kutoa
mafunzo ya kilimo shadidi kitakachoongeza kipato na uzalishaji kwa
wakulima hao.
Amesema skim hiyo ni kubwa kwa kanda ya
Magharibi hivyo wakulima hao hawana budi kuzingatia mafunzo waliyopewa ya
kilimo shadidi ambacho kitawaletea mafanikio makubwa.
''Wakulima napenda kuwaasa kuwa baada
ya kupata mafunzo sasa mbadilike msilime
kilimo cha mazoea limeni shadidi mtakuwa matajiri wakubwa hasa wa mpunga kwani
kilimo ndio kila kitu.'' amesema mkuu huyo wa wilaya.
Aidha Pangani ametahadharisha kuwa
miradi mingi imekuwa ikipotea baada ya wafadhili kuhitimisha ufadhili wao
na kusisitiza kuwa mradi huo unapaswa kuwa endelevu kwa wakulima hao hata baada
ya kuhitimishwa kwa ufadhili.
Mtafiti wa mazao ya mpunga Dkt. Tulole
Lugendo amesema mradi huo utakuwa
endelevu kwa kuwa umemgusa mkulima mmoja mmoja na kuongeza kuwa kituo hicho kitaufuatilia
kuona namna wakulima hao wanavyozingatia mafunzo hayo.
Mtafiti huyo amesema wakulima
walionufaika na mafunzo hayo ni zaidi ya 20 huku skim hiyo ikiwa na
wakulima zaidi ya 900 na kuongeza kuwa wakulima hao watakuwa walimu kwa
wakulima wengine.
Mwenyekiti wa ushirika wa Mwamapuli
Robert Lufunga amekipongeza kituo hicho cha utafiti kwa kutoa mafunzo hayo ambayo
yatanufaisha wakulima hao kwa kuongeza tija na hivyo kupambana na umasikini.
Mafunzo hayo yalifanyika kwenye ukumbi
wa Sakao mjini Igunga na kufadhiliwa na
serikali ya Japan na kuendeshwa na kituo cha utafiti wa kilimo Tumbi
kinachohudumia kanda ya Magharibi.
No comments:
Post a Comment