Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Sunday, January 17, 2016

WETCU Ltd KUPIGANIA KUPANDA BEI YA TUMBAKU NA KUSHUKA BEI YA MBOLEA


SHAMBA LA TUMBAKU
Na Paul Christian, Nkinga.

Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku kanda ya Magharibi WETCU Ltd kimeazimia kupigania kushuka kwa bei ya mbolea na kuongezeka kwa bei ya Tumbaku ili mkulima anufaike na zao hilo. 

Azma hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama hicho Mkandala Gabrie Mkandala alipofanya mahojiano maalumu na VOT FM STEREO akiwa kwenye hospitali ya rufaa Nkinga wilaya ya Igunga mkoani Tabora.

Amesema lengo la Chama hicho kwa sasa nikuhakikisha mkulima wa zao hilo anapata unafuu wa bei ya mbolea ili aweze kulima kilimo chenye tija kwa kuwa hilo linawezekana.

Mkandala amebainisha kuwa azma ya WETCU Ltd kwa sasa ni kupigania bei ya Tumbaku ipande kutoka hapa ilipo sasa hali itakayomfanya mkulima kuona mapato yanaendana na uwekezaji wa nguvu, akili, muda na fedha katika kilimo cha Tumbaku.

Aidha mwenyekiti huyo amesema kwa mwaka huu WETCU Ltd imejipanga kumfanya mkulima wa zao hilo kuendana na kalenda ya zao kwa kuanza masoko mapema ili yakamilike kati ya mwezi wa sita na wa saba.

Mkandala amesema masoko yakikamilika mapema wataweza kujua idadi na mahitaji ya Vyama vya Msingi vya Ushirika hatua itakayosaidia kuvipelekea mbolea mapema kati ya mwezi wa Nane au wa  Tisa.

Amesisitiza kuwa WETCU Ltd imejipanga kuondoa kero ya ucheleweshaji wa pembejeo kwa wakulima wa zao hilo jambo linalowaumiza sana.

Mwenyekiti huyo wa WETCU Ltd amebainisha kuwa tayari kiwanja kilichotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha Tumbaku wilayani Urambo kimepitishwa na wizara husika na hivyo kuwafanya waanze mchakato wa ujenzi.

Ametaja baadhi ya mikakati ya uwekezaji inayotarajiwa kuanza utekelezaji wake mwaka huu kuwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la ghorofa WETCU Plaza ambalo litakuza mapato ya chama hicho.

No comments: