Na Paul Christian, Kigwa.
Timu za soka za wilaya ya Uyui mkoani Tabora zilizofuzu
kushiriki ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa zimetakiwa kujianda kwa mazoezi,
kisaikolojia,kuzielewa na kuzitafsiri sheria za mchezo huo ili kuondoa
malalamiko yasiyo na msingi.
Agizo hilo limetolewa na Mbunge wa jimbo la Igalula
ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha soka wilaya ya Uyui Musa Ntimizi wakati akikabidhi zawadi kwa
washindi wa ligi daraja la nne wilayani humo iliyomalizika mwishoni mwa wiki ambapo Kigwa FC waliibuka washindi.
Mbunge huyo amesema timu hizo zikijiandaa vyema
zitaenda kushindana na sio kushiriki katika ligi daraja la tatu kwa kuwa
wanakwenda kukutana na waamuzi wenye uzoefu na waliobobea kwenye mchezo huo.
Katika hafla hiyo fupi Musa Ntimizi alitoa zawadi
ya shilingi 250,000/- na Kombe kwa timu ya Kigwa FC ambayo iliibuka kinara wa
ligi daraja la nne wilayani humo baada ya kuichapa pasipo huruma timu ya Wembe
FC ya kata ya Usagari kwa jumla ya mabao 6 kwa 2 kwenye mechi ya fainali.
Hata hivyo waswahili walisema mgaa gaa na upya
hali wali mkavu Wembe FC ilizawadiwa shilingi 150,000/- kwa kushika nafasi ya
pili huku Manchester United ya Igalula ikiambulia shilingi 100,000/- kwa kuwa
washindi watatu.
Aidha Musa Ntimizi ametoa zawadi ya mipira yenye
kiwango na ubora unakubaliwa na shirikisho la soka Duniani FIFA kwa timu zote
zilizofuzu kushiriki ligi daraja la tatu pamoja na kuahidi kuzilipia ada ya
ushiriki wa ligi hiyo.
Mbogo Zyagi mchezaji wa nafasi ya ushambuliaji wa
timu ya Kigwa FC aliibuka mfungaji bora kwa kuzifumania nyavu mara 11
alipokutana na timu pinzani tangu kuanza kwa ligi hiyo Januari 6 mwaka huu na
alizawadiwa shilingi 50,000/- taslimu.
Awali hafla hiyo ya kutoa zawadi ilitanguliwa na
mechi ya fainali iliyozikutanisha Kigwa FC na Wembe FC ya kata ya Usagari jimbo
la Tabora Kaskazini ambapo Wembe ulikosa makali na kukubali kichapo cha mabao 6
kwa 2 kutoka kwa Kigwa FC.
Magoli ya Kigwa FC yalipachikwa nyavuni na Mbogo
zyagi magoli 3, Hassan Juma goli 1, Devid Eliasi goli 1 na Ali Kassimu goli 1
na yale ya upande wa Wembe FC yalifungwa na Seleman Salum na Hamis Maige.
Ligi hiyo ya daraja la nne imegharimu kiasi cha
shilingi milioni 6 zilizotolewa na Mbunge wa Igalula Musa Ntimizi ambazo
ziligharamia ada za timu zote 13 zilizoshiriki, gharama za usafiri, gharama za
waamuzi kutoka Tabora manispaa, gharama za mipira, kombe , gharama za maofisa
wasimamizi wa ligi hiyo na nyingine.
Wilaya ya Uyui itawakirishwa na jumla ya timu 5
katika ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa ambapo Kigwa FC,Wembe FC na Manchester
United ya Igalula zinaungana na timu nyingine mbili ambazo ziko katika ngazi
hiyo ya daraja la tatu.
No comments:
Post a Comment