Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Monday, January 25, 2016

KAYA 30 ZAKUMBWA NA MAFURIKO KITONGOJI CHA USWAHILINI TARAFA YA ULYANKULU


Na Paul Christian, Kaliua.

Wakazi wa kitongoji cha Uswahilini kijiji cha Ibambo kata ya Mwongozo  wilayani Kaliua wamekumbwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika maeneo hayo na kuharibu vitu mbalimba ikiwemo nyumba, chakula na mazao kwenye mashamba.

Akizungumza na VOT FM STEREO kwa njia ya simu mwenyekiti wa kijiji cha Ibambo  Ngomba R. Ngomba amesema mafuriko hayo yamezikumba nyumba 30 na kumi kati ya hizo zimeharibiwa vibaya.

Amesema nyumba hizo 10 zilizoharibika zilikuwa zikikaliwa na  watu 90 ambao  kwa sasa wamehifadhi na majirani.

Ngomba amebainisha kuwa mafuriko hayo yameharibu chakula kilichokuwa kimehifadhiwa katika nyumba hizo hali inayosabisha familia hizo kuhitaji msaada wa dharura wa  chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa mafuriko hayo yameharibu mimea mashambani ikiwemo mpunga ekari 60, mahindi ekari 30,viazi vitamu ekari 15, karanga ekari 22, tumbaku ekari 3, mihogo ekari 1, alizeti ekari 1 na kunde ekari 5.

Ameyataja madhara mengine yaliyojitokeza ni uharibifu wa chakula kilichokuwa kimehifadhiwa kwenye kaya zilikumbwa na mafuriko kuwa ni magunia 24 ya mpunga, mahindi magunia 30, viazi vitamu vilivyokaushwa (matobolwa) magunia 20,karanga magunia 13, magunia matano ya maharage, kilo 400 za mchele na magunia matatu ya kunde.

Ngomba ameyataja madhara mengine yaliyosababishwa na mafuriko hayo ni vifo vya ng’ombe wawili na mbuzi watatu.

Mwenyekiti huyo wa kijiji cha Ibambo amesema tathimini ya uharibifu wa mazao na chakula imejumuisha kaya na maeneo yote yaliyoathiriwa na mafuriko katika kitongoji cha Uswahilini.

Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa kamati ya maafa ngazi ya wilaya ya Kaliua kuwapelekea msaada wa chakula na mahitaji mengine ya ziada wakazi hao walioathirika na mafuriko.

Wakati huo huo mto Wala umefurika maji katika eneo la Kasisi kata ya Pangale wilaya ya Sikonge mkoani Tabora na kusababisha eneo la daraja katika eneo hilo kuharibika na kusababisha magari ya abiria na mizigo yanayotumia barabara ya Tabora-Sikonge kukwama katika eneo hilo.

No comments: