.................Tulipoishia sehemu ya kwanza ya simulizi hii ya kihistoria watekaji wakaongeza siku za mazungumzo na kwamba siku ya mwisho ya
utekelezaji wa madai yao ikawa majira ya mchana ya tarehe 4 Julai, 1976. Sasa endelea.....................
![]() |
MAKOMANDOO WA ISRAEL |
Paul Christian, Tabora.
OPERESHENI ENTEBBE
Siku hiyo hiyo
ya Tarehe 1 Julai, 1976 kwa mara nyingine Watekaji waliwaachia huru mateka
wengine 100 wasiokuwa raia wa Israel ambao walisafirishwa kuelekea Paris,
Ufaransa.
Mateka 106
waliendelea kushikiliwa wakiwemo wafanyakazi 12 wa ndege hiyo ya Air France 139,
10 wakiwa vijana Wakifaransa na 84 Raia wa Israel au wenye asili ya Israel.
Serikali
ya Israel ilijaribu mara kadhaa kufanya majadiliano ya kisiasa ili mateka hao waachiliwe
huru.
Hata hivyo baraza la mawaziri la Israel lilikuwa
limejiandaa kuwaachia huru wafungwa wakipalestina wapatao 40 endapo ufumbuzi wa
kijeshi usingeonekana kufanikiwa.
Afisa mstaafu wa Jeshi la Israel IDF Baruch “Burka”
Bar Lev alikuwa akifahamiana na Idd Amin kwa miaka mingi na alidhaniwa kuwa na
uhusiano wa kibinafsi na kiongozi huyo wa Uganda.
Kwa maombi ya baraza la mawaziri la Israel afisa
huyo alifanya mazungumzo kwa njia ya simu mara kadhaa na Idd Amin ili kujaribu kufikia muafaka wa
kuachiliwa huru kwa mateka hao lakini
hakufanikiwa.
Serikali ya Israel iliiomba serikali ya Marekani imshawishi
Rais wa Misri Anwar Sadat azungumze na Idd Amin kwa ajili ya kuachiliwa huru
kwa mateka wa Israel.
Siku ile ya Julai 1, 1976 serikali ya Israel iliomba
ipewe muda zaidi wa mazungumzo, na watekaji kutoa siku ya mwisho kuwa tarehe 4
Julai 1976, Rais wa Uganda Idd Amin aliwashawishi watekaji hao kukubaliana na ombi la Israel.
Idd Amin alifanya hivyo kwa kuwa alikuwa na safari
ya kidplomasia kuelekea Port Louis
nchini Mauritius ambapo angekabidhi uenyekiti wa Umoja wa nchi za Afrika OAU
kwa Seewoosagur Ramgoolam.
Kuongezwa kwa muda wa mwisho hadi Julai 4, 1976
kulitoa fursa kwa jeshi la Israel kuvamia Entebbe.
Mnamo tarehe 3 Julai, 1976 majira ya saa 12:30 jioni
Baraza la Mawaziri la Israel liliridhia mpango wa jeshi la nchi hiyo kwenda
kuwakomboa mateka wa Israel katika ardhi ya Uganda.
Mpango wa uvamizi uliwasilishwa kwenye baraza hilo na
Meja Jenerali Yekutiel “Kuti” Adam pamoja na Brigedia Jenerali Dan Shomron.
Brigedia Jenerali Shomron aliteuliwa kuwa kamanda wa
opereseni hiyo ya kijeshi.
Licha ya mpango huo wa siri wa serikali ya Israel, Rais wa Misri Anwar Sadat alijaribu kufanya
mazungumzo na uongozi wa Chama cha Ukombozi wa Wapalestina PLO pamoja na
serikali ya Uganda.
Mwenyekiti wa PLO Yesser Arafat alimtuma mjumbe wake
Hani al-Hassan kwenda Uganda kuzungumza na watekaji pamoja na Rais wa nchi hiyo
Idd Amin, hata hivyo watekaji hao wa kundi la PFLP-EO walikataa kuonana na
mjumbe huyo wa Arafat.
Baada ya serikali ya Israel kushindwa kupata
ufumbuzi wa kisiasa dhidi ya madai ya Watekaji ili wawachilie huru mateka
waliokuwa wakiwashikilia, serikali hiyo iliamua kutumia mbinu za kijeshi.
Luteni Kanali Joshua Shani, alipewa usukani wa
kuongoza operesheni hiyo ambapo mwanzoni jeshi la Israeli lilipanga kudondosha
makomandoo ziwa Victoria na kisha kutumia boti zilizotengenezwa kwa plastic kuelekea kwenye
Uwanja wa Ndege wa Entebbe ulioko kando ya ziwa hilo.
Kwenye mpango huo walipanga kuwaua watekaji na kuwakomboa
mateka wote na baadae kumuomba Rais wa Uganda Idd Amin njia ya kuondoka
kuelekea Israel.
Hata hivyo mpango huo wa awali ulifutwa kwa sababu ulihitaji muda mwingi na jeshi halikuwa na
muda wa kutosha, na pia uwepo wa mamba kwenye ziwa Victoria.
Aidha jeshi la Israel katika uvamizi huo lilifikiria mahali pa kutua
na kujaza mafuta ndege zake aina ya Lockheed C-130 Hercules ambazo zilipangwa kutumika kwenye uvamizi huo
wa Entebbe, Uganda.
Hiyo ilikuwa changamoto kwa jeshi la Israel kwa kuwa
walihitaji msaada kutoka kwenye moja ya nchi za Afrika Mashariki na hususani
Kenya.
Mataifa ya Afrika Mashariki hayakuwa tayari
kuujingiza kwenye mgogoro na Idd Amin au Wapalestina kwa kuisaidia Israel
kutumia viwanja vya ndege ndani ya mipaka ya nchi hizo.
Jeshi la Israel lilitambua lisingeendelea na mpango
wake pasipo kupata msaada wa nchi mojawapo ya Afrika ya Mashariki.
Mmiliki wa hotel maarufu za Block hotels chain nchini
Kenya na raia wa Israel akishirikiana na wenzake wenye asili ya Israel jijini
Nairobi walitumia ushawishi wa kisiasa na kiuchumi kumshawishi Rais wa Kenya
Mzee Jomo Kenyatta kuisaidia Israel.
Hatimaye Israel ikapewa ruhusa kutoka serikali ya
Kenya kwa ajili ya jeshi lake kutumia anga na kujaza mafuta kwenye uwanja wa
ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Aidha Waziri wa kilimo wa Kenya Bruce McKenzie
alimshawishi Rais Kenyatta kuliruhusu shirika la kijasusi la Israel Mossad kukusanya
taarifa muhimu kabla ya jeshi la Israel kuvamia Entebbe.
Shirika hilo la kijasusi la Israel lilitoa picha
kamili ya mahali walipo mateka, idadi ya watekaji, silaha walizonazo watekaji
na namna jeshi la Uganda lilivyojihusisha na mgogoro huo.
Mossad ilipata taarifa za kijasusi kutoka kwa mateka
wasio waisrael ambao walioachiwa huru na kusafirishwa hadi Paris nchini
Ufaransa.
Shirika hilo pia lilitumia taarifa za makampuni ya
ujenzi ya nchini Israel ambayo yalishiriki katika ujenzi wa majengo mbalimbali
barani Afrika katika miaka ya 60 na 70.
Mossad iliwasiliana
na kampuni kubwa ya ujenzi nchini humo Solel Boneh ambayo ilijenga jengo ambalo
mateka wenye asili ya Israel walikuwa wakishikiliwa kwenye uwanja wa Entebbe
nchini Uganda.
Wakati wakipanga kutekeleza operesheni hiyo, jeshi
la Israel likisaidiwa na raia wa nchi hiyo walioshiriki kujenga jengo la
Entebbe, lilijenga jengo la muda la mfano lililofanana na lile la Entebbe
lililokuwa na mateka.
.................Usikose sehemu ya tatu ya simulizi hii ya kusisimua
No comments:
Post a Comment