Na Paul Christan, Tabora.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu Cha Ushirika wa Wakulima
wa Tumbaku Kanda ya Magharibi WETCU Ltd Mkandala Gabriel Mkandala amefanyiwa
upasuaji wa mguu wake wa kushoto kufuatia ajali aliyoipata Januari 6 mwaka huu.
Akizungumza na VOT FM STEREO akiwa kitandani
alipolazwa kwenye hospitali ya rufaa ya Nkinga wilayani Igunga mkoani Tabora
mwenyekiti huyo amesema upasuaji huo umefanyika Alhamisi wiki hii kuanzia
majira ya saa saba mchana hadi saa mbili usiku.
Mkandala amebainisha kuwa upasuaji huo umefanyika
baada ya mguu huo wa kushoto kuvunjika katika tukio hilo la ajali ambapo gari
yake iliyokuwa ikitokea Usoke wilayani Urambo kuelekea Tabora mjini kuligonga
trekta ambalo halikuwa na taa wala kiakisi mwanga katika maeneo ya Tumbi
barabara kuu ya Tabora- Urambo.
Aidha mwenyekiti huyo amesema katika ajali hiyo
pia alivunjika mkono wake wa kushoto mara mbili ambao nao utafanyiwa upasuaji
siku chache zijazo baada ya kupona majeraha yaliyotokana na kuchomwa na vyuma pamoja
na vioo.
Amesema, “tukiwa tumelikaribia trekta lile ghafla
nikaijiwa na fikra kuwa tunakwenda kuligonga nikamwambia dereva tunagonga,
lakini katika dakika hiyo hiyo nikasikia kishindo kikubwa.”amesema Mkandala.
Mwenyekiti huyo wa WETCU Ltd amebainisha kuwa
wakati ajali inatokea alikuwa na akili zake timamu licha ya kuwa alibanwa kiasi
cha kuhitaji msaada wa kutolewa aliweza kupiga simu kwa mkuu wa mkoa Ludovick
Mwananzila na familia yake kuwajulisha tukio hilo.
“Jambo la kushangaza dakika chache baada ya ajali
kutokea walifika majirani zangu wawili ambao ninaishi nao nyumbani Usoke hali
iliyonipa matumaini ya kuwa salama zaidi japo nilikuwa bado nimenasa kwenye
gari.”ameeleza Mkandala.
Amesema, “kama binadamu ninapaswa kumshukuru mungu
kwa kila jambo hata kwa hili namshukuru mungu.”
Mwenyekiti huyo amewashukuru wakulima wa Tumbaku,mkuu
wa mkoa wa Tabora Ludovick Mwananzila, Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora,
Madaktari wa hospitali ya mkoa wa Tabora Kitete, Madaktari wa hospitali ya
Rufaa Nkinga, wajumbe wa bodi na watumishi wa WETCU Ltd, Wadau wa Tumbaku,
viongozi wa vyama vya siasa na serikali pamoja na Ndugu Jamaa na Marafiki kwa
kumuombea, kumpa pole na kumjulia hali.
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa moja na nusu
usiku siku ya Jumatano ya tarehe 6 mwezi huu katika eneo hilo la Tumbi Manispaa
ya Tabora.
No comments:
Post a Comment