Na Paul Christian, Ulyankulu.
Mto Igombe uko kwenye hatari ya kutoweka kutokana
na vitendo vya uharibifu wa mazingira.
Afisa mhifadhi wanyamapori wa pori la akiba la Kigosi
Moyowosi kanda ya Kusini mkoani Tabora Thomas Mgeta Jumbula ametoa maelezo hayo
wakati wa kikao cha kazi pamoja na Mbunge wa jimbo la Ulyankulu wilaya ya
Kaliua John Peter Kadutu alipotembelea taasisi hiyo.
Amesema wakazi wa vijiji vinavyozunguka pori hilo
la akiba wamekuwa wakifanya shughuli za kilimo ndani ya mto Igombe hali inayohatarisha
uwepo wake.
Afisa huyo ametaja vitendo vingine
vinavyohatarisha mto huo ni wafugaji kulishia mifugo yao ndani ya mto huo na
ndani ya hifadhi licha ya sheria kukataza vitendo hivyo.
Thomas ametoa mfano wa mkazi mmoja wa kijiji kimojawapo kinachopakana
na pori hilo la akiba alithubutu kujenga ndani ya mto huo.
Afisa huyo amelalamikia viongozi wa serikali za vijiji
hivyo vya jirani kutotoa ushirikiano kwa
maofisa hao wahifadhi katika kuwabaini na kuwachukulia hatua waharibifu hao hali
inayosababisha ugumu katika kukabiliana na vitendo hivyo.
Amesema mto huo ni muhimu sana kwa maisha ya wanyama na viumbe hai waliopo
katika pori hilo la akiba na kwamba ukitoweka utaharisha maisha ya viumbe hao.
Akizungumzia suala hilo mbunge wa Ulyankulu John
Peter Kadutu amesema ni wajibu wa viongozi wa serikali za vijiji vinavyozunguka
pori hilo kuheshimu sheria na kuacha tabia ya kushirikiana na watu wanaovunja
sheria kwa kufanya shughuli za kilimo, uvuvi, uwindaji, upasuaji mbao au
kuchoma moto maeneo ya hifadhi.
Amesema viongozi hao wa vijiji wanapaswa
kutekeleza majukumu yao kwa kuacha kupokea rushwa au hongo kutoka kwa watu
wanaovamia hifadhi hiyo kwa lengo la kulima au kuchungia mifugo.
Hata hivyo Kadutu amewataka maofisa hao uhifadhi
wa pori la akiba la Kigosi Moyowosi kanda ya Kusini kutoa elimu kwa jamii
kuhusu uhifadhi na pia kusaidia shughuli za kijamii katika maeneo yao hali
itakayosaidia kukuza ushirikiano katika kulinda na kuendeleza pori hilo la
akiba.
No comments:
Post a Comment