Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Sunday, January 31, 2016

MTUMISHI WA AFYA AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA RUSHWA.






Na, Thomas Murugwa, Nzega.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU hatimaye imemfikisha mahakamani  muuguzi wa hospitali ya wilaya ya Nzega  John David Sambo akituhumiwa kwa makosa mawili ya kushawishi na kupokea  rushwa.

Sambo alipandishwa kizimbani  Ijumaa  mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya hiyo Seraphine Benard na kusomewa mashitaka hayo na mwanasheria wa TAKUKURU  Edson Mapalala.

 Wakili huyo wa TAKUKURU aliiambia mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa huyo alitenda makosa hayo mawili kati ya Januari 18 na  19 mwaka huu akiwa kwenye kituo chake cha kazi hospitali ya wilaya ya Nzega.

Mapalala alidai kuwa tarehe 18 Januari,2016  mtuhumiwa aliomba apewe shilingi laki moja toka kwa Suleiman Masele ili aweze kumfanyia upasuaji mdogo baba yake mzazi aitwaye Omary Masele.

Ilidaiwa katika shitaka la pili kuwa muuguzi huyo akiwa ni mtumishi wa umma alipokea shilingi elfu themanini  toka kwa Suleiman ili kiwe kishawishi cha kumfanyia upasuaji baba yake mzazi  aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa henia (ngiri).

Mtuhumiwa alikana  makosa hayo na yupo nje kwa dhamana   hadi hapo tarehe 5 mwezi huu  kesi hiyo itakapotajwa tena ili aweze kusomewa maelezo ya awali kwa kuwa upelelezi kesi hiyo umekamilika.


No comments: