![]() |
Mh. Mbunge John Peter Kadutu akizungumza na askari wa kituo cha Ulyankulu |
Na Paul Christian,Ulyankulu
Askari polisi wa kituo cha Ulyankulu wilaya ya
Kaliua mkoani Tabora wamelalamikiwa kudai malipo ya shilingi 300,000/= kutoka
kwa wananchi kama gharama ya mafuta ya kuwafikisha kwenye matukio ya kihalifu.
Akizungumza na askari hao mbunge wa jimbo la
Ulyankulu John Peter Kadutu amesema hivi karibuni askari hao walidai wapewe
kiasi hicho cha fedha ili waweze kufika kijiji cha Sasu kulipotokea uhalifu.
Amesema kitendo cha kudai fedha kutoka kwa
wananchi ili watekeleze majukumu yao ni miongoni mwa kero walizonazo wananchi
wa jimbo hilo dhidi ya askari hao.
Kadutu amewataka askari hao kuacha kuwaomba fedha
wananchi kwa kuwa ni ukiukaji wa sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza
shughuli za utekelezaji wa majukumu yao.
Mbunge huyo ameweka bayana kuwa endapo askari hao
watatenda haki kwa kuacha kuwaonea wananchi kwa kuwaomba fedha za mafuta,
kupokea rushwa na kuwabambika kesi hawataingiliwa katika kutimiza majukumu yao.
Kadutu amebainisha kuwa kila mkazi wa jimbo hilo
angependa kuishi kwa amani na utulivu huku akijikita zaidi kwenye shughuli za
uzalishaji mali badala ya kuhangaikia kesi za kutengenezwa na askari hao kwa lengo
la kujipatia fedha isivyohalali.
Amesema, “kumekuwa na malalamiko mengi juu yenu
jambo ambalo linapaswa kuangaliwa kwa kutekeleza majukumu yenu kwa mujibu wa
taratibu zenu badala ya kutanguliza tamaa ya kujinufaisha.”
Mbunge huyo wa Ulyankulu amewahimiza askari hao
kuacha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kuwapiga watuhumiwa au
kuwanyanyasa kwa namna yoyote hata kama wametii kuwa chini ya ulinzi.
Kadutu amebainisha kuwa vitendo hivyo vinazidi
kuchochea chuki kutoka kwa wananchi hali ambayo inadhoofisha dhana nzima ya polisi
jamii, ulinzi shirikishi na utii wa sheria pasipo shuruti.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya ya Kaliua Haruna Kasele amekemea tabia ya baadhi ya askari hao kuvujisha
siri wanazopewa na raia wema kuhusu uhalifu au wahusika wa uhalifu kwa nia ya
kujinufaisha.
Amesema tabia hiyo ni kinyume na maadili ya jeshi
la polisi na imewafanya wananchi kujitojihusisha na jeshi hilo katika kusaidia
kupambana na uhalifu katika jimbo hilo la Ulyankulu.
Mbunge wa Ulyankulu John Peter Kadutu amefanya
ziara ya siku ya tatu ya kutembelea taasisi za umma na binafsi kwa lengo la
kupokea ushauri, kero na maoni kabla ya kuanza vikao vya bunge Januari 26 mwaka
huu.
No comments:
Post a Comment