![]() |
BAADHI YA WATUMISHI WA KITUO CHA AFYA ULYANKULU WILAYA YA KALIUA MKOANI TABORA |
Na Paul Christian, Ulyankulu.
Halmashauri
ya wilaya ya Kaliua mkoani Tabora imelalamikiwa kutowalipa malipo ya kazi za
ziada watumishi wa kituo cha afya Ulyankulu wanapoambatana na wagonjwa wa rufaa
kuwapeleka hospitali ya wilaya ya Urambo au kwingineko.
Watumishi
hao wametoa malalamiko hayo hivi karibuni kufuatia mbunge wa jimbo la Ulyankulu
John Peter Kadutu kufanya ziara ya kikazi katika kituo hicho kinachohudumia
wakazi wa kata 18 za tarafa ya Ulyankulu wilayani humo.
Wamesema walipokuwa chini ya halmashauri ya wilaya ya Urambo walikuwa wakilipwa
malipo ya kazi za ziada jambo ambalo halifanyiki katika halmashauri ya wilaya
ya Kaliua.
Afisa
muuguzi Fatuma Shaban amebainisha kuwa kutokana na kituo hicho kukabiliwa na
upungufu wa watumishi wanalazimika kufanya kazi hadi saa za ziada lakini
wanapoomba kulipwa fedha za muda huo wamekuwa wakilipwa kidogo na yanachukua
muda mrefu.
Naye
dereva wa gari la wagonjwa Adrey Mkini ameitaka halmashauri hiyo iwe inamlipa
madai yake ya kazi za ziada ndani ya muda mfupi baada ya kuwasilisha madai yake
ili aweze kupata fedha za kulihudumia gari hilo.
Amesema,
“Gari linapopata pancha au matatizo mengine madogo madogo ni malipo hayo ya
kazi za ziada nayatumia kulihudumia.”
Aidha
muuguzi Shida Juma Katindili ameitaka halmashauri hiyo kuwapatia sare angalau
mara mbili kwa mwaka kwa kuwa wanapata shida kuvaa sare moja kwa mwaka mzima.
Mtaalamu
wa maabara Josia Raphael Bitulo ameitaka idara ya afya kuwatimizia mahitaji ya
vifaa tiba vya maabara kulingana na maombi yao ili waweze kutoa huduma yenye
tija kwa wagonjwa.
Mlinzi
wa kituo hicho Simon Kamugwa amesema amekuwa akifanya kazi ya ulinzi peke yake
tangu mwaka 2012 baada ya mwenzake kustaafu hali inayomsababisha kufanya kazi
hata wakati akiwa anaumwa.
Mlinzi
huyo ameitaka halmashauri hiyo kuongeza walinzi kwa kuwa kituo hicho ni kikubwa
na kina mali nyingi ikiwemo gari la wagonjwa.
Akijibu
madai hayo ya watumishi, mwenyekiti wa kamati ya huduma ya afya, Elimu na Maji
kwenye halmashauri ya wilaya ya Kaliua Alphonce Msanzya amesema madai yote
wameyachukua na wanakwenda kuyafanyia kazi.
No comments:
Post a Comment