Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Sunday, January 3, 2016

WAWILI KIZIMBANI KWA KUGHUSHI, KUTUMIA MADARAKA VIBAYA.



Na, Thomas  Murugwa, Tabora.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imewafikisha mahakamani watu wawili kwa tuhuma tofauti  mmoja kwa kuhujumu uchumi  na mwingine kughushi nyaraka hivyo wote  kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.

Waliofikishwa mahakamani  ni aliyekuwa afisa misitu  msaidizi wa wilaya ya Sikonge  Krety John ambaye anakabiliwa na mashtaka saba ya kutumia madaraka vibaya na Cathberth Ndogoma aliyekuwa mratibu wa  Tabora NGOS Cluster  akiwa na tuhuma 19 za kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri.

Katika kesi inayomkabili  Krety John ilidaiwa na wakili wa TAKUKURU Edson Mapalala mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Tabora Emanuel Ngigwana kuwa alitenda makosa hayo kati ya  tarehe 26 Machi 2010 na tarehe 25,2012 huko wilaya ya Sikonge na kumsababishia mwajiri hasara ya zaidi ya shilingi milioni  27.

Wakili Mapalala aliiambia mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa akiwa mtumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Sikonge kama afisa misitu msaidizi alitoa vibali vya kusafirishia mazao ya misitu kwa watu mbali mbali bila kuzingatia sheria ya misitu.

Wakili huyo alibainisha kuwa mnamo tarehe 26 Machi 2010 mtuhumiwa kwa makusudi alitoa kibali chenye thamani ya shilingi milioni tatu na kati ya tarehe 12 Julai na tarehe 16 Oktoba 2010 alitoa vibali vyenye thamani ya shilingi 10,052,800/- bila kuzingatia  sheria ya misitu.

Upande wa mashitaka ulidai kuwa mtuhumiwa akiwa ni mtumishi wa serikali kati ya desemba 16/2010 na machi mosi 2012 alitumia madaraka yake vibaya kwa  kutoa vibali  vyenye thamani ya shilingi milioni  14,004,000/= na kuisababishia hasara serikali.

Ilidaiwa  kwenye shitaka la saba kuwa kati ya machi 2010 na machi 2/2012 mtuhumiwa alishindwa kutimiza majukumu yake na kuisababishia serikali hasara  ya shilingi milioni 27,666,400/=.

Mtuhumiwa huyo yupo nje kwa dhamana hadi januari 11 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.

Katika kesi inayomkabili Kathberth Ndogoma ilidaiwa na wakili huyo wa TAKUKURU mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa wa Tabora Joctan Rushwela kuwa alitenda makosa hayo kati  ya tarehe 11 Novemba 2008 na tarehe 23 Disemba 2008 akiwa mfanyakazi wa taasisi ya Tabora NGOs Cluster.

Wakili Mapalala alidai kuwa katika kipindi hicho na kwa tarehe tofauti mtuhumiwa kwa lendo la kudanganya alighushi daftari la mahudhurio  likionyesha majina ya watu walihudhuria mafunzo ya utoaji huduma kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi na ukimwi majumbani.

Aliongeza kuwa mtuhumiwa pia alighushi hati mbali mbali za malipo zikionyesha kwamba amewalipa watu waliohudhuria mafunzo hayo kiasi cha shilingi elfu tano kila mmoja hivyo kuisababishia hasara Tume ya kudhibiti UKIMWI nchini TACAIDS ambayo ilitoa fedha hizo.

Mapalala alidai kuwa mtuhumiwa kwa makusudi alibadili matumizi ya fedha na kusababisha hasara  ya  shilingi milioni 6,496,000/- zilizotolewa na TACAIDS  kwa ajili ya mafunzo  ya wanaowahudumia wanaoishi na Virusi vya UKIMWI majumbani . 

Mtuhumiwa alikana tuhuma zote 19 lakini wadhamini wake walishindwa kutimiza masharti ya dhamana alipelekwa rumande hadi januari 14 mwaka kesi yake itakapoanza usikilizwaji wa awali.

No comments: