![]() |
MBUNGE WA ULYANKULU JOHN PETER KADUTU AKIZUNGUMZA NA WAFANYABIASHARA, WENYEVITI WA VITONGOJI NA VIJIJI JIMBONI HUMO |
Na Paul Christian, Ulyankulu.
Wakazi wa
tarafa ya Ulyankulu wilaya ya Kaliua mkoani Tabora wamesema wanateseka kwa
kukosa huduma za kibenki pamoja na vituo vya mafuta hali inayowafanya wasafiri
umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Kero hizo ziliainishwa na watumishi wa
umma,wafanyabiashara,vyama vya masingi vya ushirika na viongozi wa dini wakati wakizungumza kwa nyakati tofauti na mbunge wa
jimbo la Ulyankulu wilayani humo John Peter Kadutu alipofanya ziara ya kikazi jimboni
humo.
Wamesema ukosefu wa huduma za kibenki katika
tarafa hiyo unawasababisha kusafiri umbali wa kilometa 90 au zaidi kufuata
huduma hizo wilaya ya Urambo au Tabora mjini na hivyo kuwagharimu fedha nyingi
na muda mwingi ambao ungetumika kuzalisha mali.
Wakazi hao wamesema hali hiyo imewafanya
wafanyabiashara na wafanyakazi kutembea na fedha nyingi mkononi hali
inayohatarisha maisha na mali zao kwa kuwa matukio ya uhalifu yamekuwa
yakiwalenga mara kwa mara.
Wakizungumzia ukosefu wa vituo rasmi vya kuuza
mafuta ya petroli,dizeli ,mafuta ya taa pamoja na bidhaa nyingine za vyombo vya
moto wamesema taasisi za umma na binafsi zimekuwa zikipata
usumbufu kutimiza masharti ya sheria ya manunuzi kwa kuwa huduma hizo
zinapatikana zaidi ya kilometa 90 kutoka tarafa hiyo.
Aidha wakazi hao wamebainisha kuwa kero hizo ni
miongoni mwa sababu zinazowafanya watumishi wa umma kushindwa kukaa kwa muda
mrefu kufanya kazi tarafani humo.
Akijibu hoja hizo mbunge wa jimbo hilo John Peter Kadutu amewaambia
wakazi hao kuwa suala la benki linashughulikuwa kwa kuwa tayari Milambo SACCOS iliyopo barabara ya 13 tarafani humo inalo jengo
lenye miundombinu ya kibenki na kinachohitajika ni mwekezaji tu.
Mbunge huyo amesema analifuatilia suala hilo
jijini Dar es Salaam ambapo atazungumza na mkurugenzi wa benki ya CRDB ambayo ni mdau mkubwa wa SACCOS hiyo kwa kusaidia ramani ya jengo na mambo
mengine.
Kuhusu vituo vya mafuta Kadutu amesema
atalifikisha suala hilo kwa makampuni yanayofanya biashara hiyo ili kuona
uwezekano wa kuwekeza kwenye tarafa ya Ulyankulu.
Hata hivyo mbunge huyo amewatia moyo watumishi wa
umma wanaofanya kazi katika tarafa hiyo kwamba kero zilizopo sasa zimeanza
kushughulikiwa na zitatatuliwa moja baada ya nyingine.
No comments:
Post a Comment