Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Wednesday, December 30, 2015

WANANCHI WATAKA MIPAKA YA HIFADHI IWEKWE NA KUONEKANA



Na Hastin Liumba,Kaliua

WAKAZI wa kata ya Zugimlole wilaya ya Kaliua mkoani Tabora wameshangazwa na hatua ya maofisa wa maliasili kuwazuia kufanya shughuli za kilimo katika maeneo yanayodaiwa ni sehemu ya hifadhi  ya Mpanda Forest na Sawima.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa Kitongoji cha Kanyanya, kijiji cha Imbulisiasi pamoja na kitongoji cha Iga kijiji cha Uyumbu walisema hatua hiyo imeathiri uzalishaji wa chakula na hivyo kuwaweka kwenye hatari ya kukumbwa na njaa.

Wakazi hao walibainisha mazao ya chakula waliyolima katika maeneo hayo kuwa ni mahindi na mpunga kabla ya kutakiwa kusitisha shughuli hizo tarehe 12 mwezi huu. 

Aidha walieleza kuwa maofisa wa maliasili waliwanyang’anya zana zao za kilimo jambo linalowafanya washindwe kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo mengine.

Mmoja wa wakazi hao Peter Luhimba alisema serikali imeshindwa kuainisha mipaka ya hifadhi hizo jambo linalowachanganya na kushindwa kuelewa mipaka halisi ni ipi ili waiheshimu tofauti na ilivyosasa.

Sai Juma alibainisha kuwa wao kama wananchi ni sehemu ya uhifadhi wa hifadhi hizo hivyo wanapaswa kuijua mipaka pamoja na kushirikishwa ipasavyo katika ulinzi badala ya kuchukuliwa kama waharibifu.

Naye Leonard Charles alieleza kwamba hali ya kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kwenye hifadhi hizo kunawafanya baadhi ya watumishi wa maliasili kuwaonea na kuwanyanyasa wananchi kwa lengo la kujinufaisha.

Kwa kauli moja wakazi hao wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwaruhusu wahudumie mazao yao hadi yatakapo komaa  na kuvunwa ambapo watatafuta  maeneo mengine yanayofaa kwa kilimo.

wameztaja zana zao za kilimo zilizochukuliwa na maafisa hao wa maliasili kuwa ni pamoja na majembe ya mkono, matrekta na ng’ombe wanao kokota majembe ya kilimo.

Diwani wa kata ya Zugimlole Balikeka Ramadhan alipohojiwa kuhusu suala hilo alisema wananchi wake sasa hawalimi baada ya kunyang’anywa zana za kilimo.

Diwani huyo alisikitishwa na maofisa hao wa maliasili kufika katika maeneo hayo yanayodaiwa yako ndani ya hifadhi bila kushirikiana na uongozi wa kata hiyo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua Athuman Kihamia alisema
zoezi hilo halikufanywa na maofisa wa ofisi yake bali lilifanywa na wakala wa misitu nchini TSF.

Alipohojiwa Mkuu wa wilaya Kaliua Hadijah Nyembo alisema naye alisema zoezi hilo la kuwahamisha wananchi wanaodaiwa kuwa ndani ya hifadhi wahusika ni Maliasili hivyo wakiulizwa watakuwa na majibu ya msingi.

Meneja misitu wa wilaya ya Kaliua John Madohora alisema wananchi hao
ni kweli wameingia na kuvuka mipaka ya hifadhi na wanaendesha kilimo.

Madohora alisema tumekuwa tukiwaondoa kisheria na kwamba tatizo kubwa lipo kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwani wamekuwa wakichukua fedha na kuuza maeneo ya hifadhi.

Aliyataja maeneo ambayo wananchi wamevamia ni Mpanda Line kwenye maeneo ya Kangeme, Lumbe, Usinge, Ukumbisiganga na Kakole na kwamba zipo taratibu za kuangalia mipaka na kwaleza wazi kuwa wako kwenye hifadhi.

Alisema alama za mipaka zipo na zinaonekana bayana na kumekuwa na jitihada za kufyeka nyasi ili ziweze kuonekana kwa uwazi.

Madohora alisema wanasiasa wanaingilia kati kuwatetea wananchi waendelee kukaa kwenye hifadhi  lakini mamlaka inachukua hatua hizo kunusuru misitu.

No comments: