Na Paul Christian, Tabora.
Mbunge wa Jimbo la Igalula wilaya ya Uyui mkoani
Tabora ameahidi kutoa mifuko ya saruji 1,100 kwa lengo la kuchochea utekelezaji
wa miradi ya ujenzi katika kata 11 za jimbo hilo.
Ahadi hiyo ameitoa Jumatatu alipokuwa akizungumza
kwenye kikao alichokipa jina la kamati maalumu kilichohudhuriwa na Madiwani
pamoja na Watendaji wa Kata wa jimbo la
Igalula na kufanyika kwenye Ukumbi wa mikutano wa Tabora Rest House mjini
Tabora.
Ntimizi amesema mifuko hiyo 1,100 ya saruji ambayo
ni mifuko 100 kwa kila kata ameitoa kama kichocheo cha ubunifu na ufanisi wa
kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi kulingana na vipaumbele vya kata
husika.
Amebainisha kuwa licha ya kutoa mifuko hiyo 100
kwa kila kata hata sita kuongeza mifuko zaidi ya saruji pale atakapo baini
uongozi wa kata husika umesimamia vizuri miradi itakayokuwa imekusudiwa.
Mbunge huyo wa Igalula amewahakikishia wajumbe wa
kikao hicho kuwa mifuko hiyo ya Saruji 1,100 ataitoa na kuikabidhi kwao tarehe
10 ya mwezi wa Januari mwaka 2016.
Akizungumzia sekta ya afya amesema lengo lake ni
kuhakikisha anaitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayoelekeza kila kijiji kuwa
na zahanati na kila kata kuwa na kituo cha afya.
Aidha amebainisha kuwa kutokana na jiografia ya
jimbo la Igalula viongozi wa kata wanaowajibu wa kuangalia namna ambavyo kata
zinaweza kushirikiana kujenga vituo vya afya kulingana na ukaribu wa kata
husika.
Ntimizi amesema atahakikisha anapigania na kutetea
maslahi ya watendaji wa vijiji na kata kwa kuwa wanafanya kazi kubwa ya
kukusanya mapato ya Halmashauri pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo
yao.
Amesema watendaji wa kata wanapaswa kuwezeshwa
vyombo vya usafiri ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi na kwa viwango
vinavyoonekana.
Amesema Kikao hicho alichokiita kamati maalumu kitakuwa
kikikutana kila baada ya miezi minne.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Uyui, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Afisa Mipango wa
Halmashauri, wajumbe wa sekretariet ya Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Uyui
pamoja na wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM
wilayani humo.
No comments:
Post a Comment