Na, Murugwa Thomas, Tabora
MAHAKAMA KUU kanda ya Tabora imesikiliza kesi ndogo ya
kuomba kutokulipa ama kupunguziwa dhamama ya gharama ya kesi ya kupinga matokeo
ya ubunge jimbo la Tabora mjini na kwamba itatoa uamuzi Disemba 14 mwaka huu.
Hatua hiyo imefikiwa na jaji
mfawidhi wa Mahakama ya Kuu kanda ya Tabora Amir Mruma baada ya kusikiliza
maombi ya wanachama wanne wa Chama Cha Wananchi CUF waliofungua shauri hilo pamoja
na pingamizi la walalamikiwa.
Wanachama hao wakiwakilishwa na
wakili msomi wa kujitegemea Hashim Mziray
katika maombi yao wanaiomba mahakama iwakadirie kiwango waanachoweza
kulipa kama dhamana ya kesi ama iwasamehe wasilipe chochote katika shauri lao namba 3/2015 la kupinga
matokeo ya uchaguzi.
Pia wameiomba Mahakama Kuu
iwarejeshee gharama zao kwa namna itakavyona kwa kuwa wanakipato
kidogo ambacho kinawasaidia kumudu
maisha ya familia zao kwani wao ni wajasiriamali wadogo na wanawategemezi..
Aidha maombi hayo yalipingwa na mawakili Kamaliza
Kayaga anayemwakilisha mlalamikiwa wa kwanza Emanuel Mwakasaka na wakili
mwandamizi wa serikali Juma Masanja anayewawakilisha walalamikiwa wawili kwa madai kwamba hawakuleta
ushahidi wa uthibitisho kwenye maombi yao ya kiapo.
Mawakili hao walidai kuwa endapo
walalamikaji wasingekuwa na uwezo wangeenda kwenye mashirika ya msaada wa
kisheria kuomba msaada lakini wao wameweza kumkodi wakili msomi kutoka jiji Dar
es salaam hivyo wanao uwezo mkubwa wa kifedha.
Waliongeza kuwa mahakama hiyo inabidi
itilie maanani kuwa endapo walalamikaji watashindwa kesi ya msingi watashindwa
kuwalipa walalamikiwa gharama za uendeshaji wake ambazo wameisha anza kuingia
katika shauri hilo.
Kutokana na hali hiyo wameiomba
mahakama iwape nafasi kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya kesi za uchaguzi
walipe walau kiasi cha fedha kama dhamana ili kuwe na ulinganifu kama ambavyo
imefanya katika maamuzi yake kwenye kesi za aina hiyo zilikwisha funguliwa
mwaka huu.
Wananchama wanne wa Chama Cha Wananchi CUF wamefungua
kesi mahakama kuu kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Tabora mjini ambalo
Emanuel Mwakasaka wa CCM alishinda kwa kura 44,114 dhidi ya kura 35,452 alizopata Peter Mkufya wa CUF akiungwa mkono na vyama vyanavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi, UKAWA.
Wanachama hao Jumanne Mtunda,
Johari Kasanga, Thomas Omoth na Shaban Mussa wamefungua kesi hiyo Na.
3/2015 wakidai mahakama iwape haki
yao ya msingi kama wapiga kura kwa kuwarejeshea mbunge waliomchagua
Peter Mkufya.
No comments:
Post a Comment