Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Monday, December 28, 2015

SIMBA WAVAMIA MAKAZI NA KUUA NG'OMBE WANNE WILAYA YA UYUI MKOANI TABORA.




Na Paul Christian,Tabora.

Simba wanyama wamevamia makazi ya watu na kuua ng’ombe wanne katika vijiji vya Nkulusi na Ndono katika kata ya Ndono wilaya ya Uyui mkoani Tabora.

Akizungumza kwa njia ya simu leo mchana mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Uyui Said Ntahondi amesema simba hao wamewaua ng’ombe wawili katika kijiji cha Nkulusi usiku wa Jumamosi na usiku wa Jumapili wamewaua ng’ombe wengine wawili katika kijiji cha Ndono.

Amesema mnamo majira ya saa tisa alasiri leo simba hao wameonekana katika milima ya Mbola iliyopo kata ya Isila, tarafa ya Ilolangulu wilayani humo na hivyo kuwataka wakazi wa tarafa hiyo kuchukua tahadhari dhidi ya simba hao.

Ntahondi ameeleza kuwa serikali imechukua hatua mbali mbali ikiwemo askari wa wanyama pori kufanya msako dhidi ya simba hao kwa lengo la kuzuia madhara zaidi yanayoweza kutokea kwa binadamu na mifugo.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri amewataka wakazi wa kata zote za tarafa ya Ilolangulu kutembea kwa kujihami kwa kuwa na silaha za jadi kama vile mashoka, mapanga, mikuki,pinde na mishale tayari kukabiliana na wanyama hao.

Aidha Ntahondi amewataka wazazi na walezi kuwaangalia watoto wao na kuchukua tahadhari kila mahali wanapokuwa katika kipindi hiki ambacho simba hao wanatafutwa.

Amefafanua kuwa wataalamu wa wanyapori wameeleza kuwa simba wanatabia ya kutembea hadi umbali wa kilometa 50 katika uelekeo wowote kutoka mahali walipo hivyo ni muhimu kwa wananchi kuchukua tahadhari.

Ntahondi amewataka wanachi kutoa taarifa mara moja kwa watendaji wa vijiji na kata, mkuu wa wilaya ya Uyui, mwenyekiti wa halmashauri na hata kwa viongozi wengine endapo watawaona simba hao ili hatua zichukuliwe.  


No comments: