Na Paul Christian, Tabora
Hifadhi ya Taifa ya Gombe ni ya pili kwa udogo
ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 56 zilizoambaa sambamba na ziwa
Tanganyika, umbali wa kilomita 16 Kaskazini mwa mji wa Kigoma.
Hifadhi hii ni maarufu kwa wanyama adimu Sokwemtu wanaokaribiana sana na binadamu katika muundo
wa “kijenetiki” kwa zaidi ya asilimia 98.
Sokwemtu wanafanana na binadamu kwa muundo wa
ubongo na mataya yao.
Hifadhi hii yenye Sokwe waliozoeshwa kwa binadamu
imepakana na vijiji vitano vya Mwamgongo, Mtanga,Mgaraganza,Bubango na
Chankele.
Hifadhi ya Taifa ya Gombe inakadiriwa kuwa na
idadi ya Sokwe 110 ambao wamefanyiwa utafiti tangu mwaka 1960, ikiwa pori la
akiba.
Shughuli za utalii katika hifadhi hiyo zilianza
rasmi mwaka 1978 baada ya watafiti na uongozi kufanikiwa kuwazoesha Sokwemtu
kukaribiana na binadamu.
Gombe ilipandishwa hadhi na kuwa hifadhi ya Taifa
mwaka 1968 kutokana na jitihada za Jane Goodall kuanzisha kituo cha utafiti wa
Sokwemtu na mazingira yake mwaka 1965.
Utafiti wa tabia za Sokwe tangu mwaka 1960 umekuwa
ukifanyika kwa kumfuatilia kila Sokwe tangu kuamka hadi kulala pamoja na
kuratibu tabia na matukio yote ya siku.
UJIRANI
MWEMA
Kwa mujibu wa taarifa ya Mhifadhi mkuu wa Hifadhi
ya Gombe, Noelia Myonga.
Hifadhi ya Taifa ya Gombe imesaidia miradi
mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wa Kigoma katika kuimarisha ujirani mwema.
Hifadhi imesaidia mradi wa kuimarisha mazingira ya
chanzo cha maji cha Mgaraganza, ujenzi wa kituo cha polisi cha mpakani Kagunga
na ujenzi wa maktaba ya wilaya ya Kasulu.
Aidha hifadhi imesaidia ujenzi wa bweni la
wasichana shule ya sekondari ya Bugamba na vyumba vinne vya madarasa katika
shule ya sekondari ya Kagongo.
Hifadhi inatarajia kutekeleza miradi ya ujenzi wa
bweni la wasichana shule ya sekondari
Bitale, na uvunaji wa umeme jua kwa vikundi vya uvuvi vya Mwamgongo na
Mtanga kwa mwaka 2014/2015.
No comments:
Post a Comment