Na Paul Christian, Tabora.
Waandishi wa habari mkoani Tabora wanaoendelea na
mafunzo ya siku tano mjini Tabora juu ya uandishi mahiri wa habari za uchunguzi
wamekumbana na changamoto ya kung’amua misamiati inayotumika kwenye taaluma
mbalimbali ikiwemo Uhasibu.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo Mwandishi Mwandamizi,
Fili Karashani aliwataka waandishi hao kung’amua tafsiri ya misamiati hiyo ya
kitaaluma kwa kutoa zoezi la tafsiri sahihi juu ya maneno kadhaa ya kiingereza.
Alisema kila mmoja wenu atafsiri misamiati hii, “Unqualified financial audit report na negative response.”
Msamiati wa Negative response ulipatikana katika
sentensi iliyosomeka, “He said, I applied for the job and I got a negative
response.”
Lengo la mwezeshaji huyo lilikuwa ni kupima
umakini wa waandishi hao wa habari katika kung’amua vitu mbalimbali kwa umahiri
na usahihi wakati wa wakufuatilia habari za uchunguzi.
Karashani alitoa majibu ya zoezi hilo kuwa karibu
waandishi wote walibaini katika sentensi hiyo ya kiingereza kuwa mkazo uliwekwa
kwenye maneno “negative response”.
Aidha Mwezeshaji huyo alitoa zoezi lingine ambalo
liliwataka waandishi hao kung’amua tafsiri sahihi ya Kiswahili ya maneno “unqualified financial audit report.”
Baada ya dakika 6 hivi, Karashani alitoa majibu ya
zoezi hilo ambayo yalibaini kuwa waandishi wengi walieleza tafsiri ya maneno “unqualified financial audit report” kuwa ni hati
isiyoridhisha au chafu inayotolewa na mkaguzi wa mahesabu jambo ambalo halikuwa
sahihi.
Mwezeshaji huyo alimtangaza mwenyekiti wa Tabora
Press Club Teonest Liwa kuwa mwandishi pekee aliyejibu kwa ufasaha zoezi hilo kwa
kutoa tafsiri ya maneno, “unqualified financial audit
report” kuwa ni hati safi
inayotolewa na mkaguzi wa mahesabu.
Aliongeza kuwa katika uhasibu neno “unqualified” linamaana ya safi au inayoridhisha hivyo
ni lazima kuongeza maarifa ya kujua kwa ufasaha misamiati ya kitaaluma ili iwe
rahisi kuandika habari za uchunguzi katika kiwango cha uandishi uliotukuka.
Leo waandishi hao wanafanya mazoezi kwa vitendo
kwa makundi yaliyopewa majina ya kubuni ya vyombo vya habari ambavyo ni the Mirror,Hapa
Kazi Tu,Tabora leo na Kagera Raha.
Mafunzo hayo ya siku tano yalianza siku ya Jumanne
na yatakamilika Jumamosi katika ukumbi wa mikutano wa hosteli ya
Moravian mjini Tabora.
No comments:
Post a Comment