Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Monday, December 14, 2015

KESI YA KUPINGA MATOKEO YA UCHAGUZI JIMBO LA TABORA MJINI.





Na,  Murugwa Thomas, Tabora.

Mahakama Kuu kanda ya Tabora imewataka wananchi wanne waliofungua kesi ya kupinga matokea ya uchaguzi jimbo la Tabora mjini kulipia shilingi milioni tisa kama dhamana ndipo shauri hilo liweze kusikilizwa.

Uamuzi huo umetolewa jana na jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Tabora Amir Mruma baada ya kusikiliza maombi ya wananchama hao wanne wa Chama cha Wananchi CUF waliowakilishwa na wakili wa kujitegemea Hashim Mziray kutoka jijini Dar es salaam.

Katika kesi hiyo  ya madai na 49/2015 ya kuomba kupunguziwa gharama ya dhamana ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakama hiyo imeamuru kila mlalamikiwa alipiwe dhamana ya shilingi milioni tatu.

Jaji Mruma alisema kuwa katika kesi za uchaguzi sheria inaitaka Mahakama iangalie ni kiasi gani cha fedha mlalamikaji alipe kama dhamana bila kujali uwezo alionao.

Aliongeza kuwa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga sheria ya gharama za kesi za uchaguzi kwa lengo la kupunguza kufunguliwa kwa mashauri mengi yasiyo na msingi.

Jaji  Mruma katika uamUzi wake huo amesema kuwa  amepitia maelezo ya pande zote mbili  na kuridhika na upande wa wajibu maombi kuwa walalamikaji wanaouwezo mkubwa kifedha hivyo wanapaswa kulipa dhamana ya shilingi milioni  15 ili  kesi ya msingi iweze kusikilizwa.

Akifafanua zaidi jaji huyo alisema kuwa walalamikaj wameshindwa kuleta uthibitisho wa kuunga mkono  maombi yaliyoainishwa katika hati za viapo vyao  kwamba wao ni masikini na kwamba hawataweza kumudu kulipa kiasi hicho cha fedha kama dhamana.

Awali upande wa wajibu maombi wakiwakilishwa na wakili Kamaliza Kayaga na Juma Masanja wakili wa serikali waliiambia mahakama hiyo kuwa waombaji wote wanne wanapaswa kuleta uthibitisho juu ya kuwa na wategemezi wengi wanaoishi nao.

Naye wakili Mziray anayewawakilisha  walalamikaji ameliambia gazeti hili kuwa ameridhika na uamzi uliotolewa na kwamba wateja wake watajipanga ndani ya siku 14 waweze kulipa kiasi kilichoamuliwa na Mahakama ili kesi ya msingi iweze kusikilizwa.

Wanachama wanne wa CUF Jumanne Mtunda, Johari Kasanga, Shaban Mussa na Thomas Ayengo wamefungua kesi mahakama kuu kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Tabora mjini yaliyompa ushindi mgombea wa CCM Emanuel Mwakasaka.

Katika shauri hilo namba  3/2015 wananchi hao wanadai uchaguzi huo haukuwa wa huru na wa haki hivyo wanaiomba Mahakama itengue matokeo yake na kumpa ushindi aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Wananchi CUF, Peter Mkufya.

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi kifungu na 111 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2015 inamtaka mtu yoyote anayefungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi alipe dhamana ya shilingi milioni 15, na  endapo akishindwa fedha hizo zisaidie kulipia gharama alizotumia mlalamikiwa.



No comments: