Mwanasayansi Muingereza Sir Isaac
Newton aliyezaliwa Januari
4,1643 na kufa Machi,31,1727
aliwahi kusema, “I can calculate the motion of heavenly bodies, but not the
madness of people.”
Kwa lugha ya Kiswahili mwanasayansi
huyo alimaanisha, kwake ilikuwa
rahisi kufanya hesabu ya mwendo wa vitu
mbalimbali, lakini kamwe asingeweza kufanya hesabu kujua kiwango cha uwendawazimu
kwa watu.
Sir Isaac Newton,ananikumbusha kuitazama serikali ya Tanzania na mkakati wake wa
makusudi wa kujenga msingi wa watu wake kuwa na Afya Bora kutokana na chakula, matunda pamoja na
vinywaji wanavyokunywa.
Tanzania imekuwa dampo la utamaduni, vyakula na vinywaji kutoka
ndani na nje ambavyo havina ubora wala umuhimu kwa afya, huku serikali ikichukua hatua hafifu kulinda afya za watu wake
kwa kuzuia uingizaji na utengenezaji holela wa vitu hivyo.
Kama Taifa nilitegemea kuona
mkakati wa vitendo usiotiliwa shaka kwa serikali kuwajenga watu wake toka
utotoni hadi uzeeni kwa kuwa na tabia ya kuzingatia lishe bora kama msingi
imara wa kuondokana na magonjwa yakitabia.
Uwendawazi anaouzungumza
mwanasayansi Sir
Isaac Newton ulionekana mwaka 2011 ilipozuka dawa ya muujiza maarufu
kama “kikombe cha babu” iliyotolewa kwa hisani ya Mchungaji mstaafu wa KKKT, Ambilikile Mwasupile katika
kijiji cha Samunge wilaya ya Loliondo.
Dawa hiyo ya kimuujiza ilidaiwa kutibu magonjwa
yote ikiwemo magonjwa sugu ya Kisukari na UKIMWI, mamia kwa maelfu ya
watanzania wakamiminika kwa babu ili waweze kupata kikombe cha dawa kwa Tshs. 500 tu.
Maajabu hayo yalikuzwa na
vyombo vya habari na kuungwa mkono na serikali ya Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa mawaziri wake akiwemo Rais wa sasa Dr. John Pombe Magufuli kukimbilia
Samunge kupata muujiza.
Jambo muhimu hapa ni kwamba dawa hiyo ya “Babu” inatokana
na mmea ambao kwa wamaasai unajulikana kama “Engamuriaki”
au “Olmuriaki” na kwa Wasonjo unajulikana
“Engamuriaga.”
Aidha
Kitaalamu mmea huo unajulikana “Carissa spinarum” ( Carissa edulis) ambao ni miongoni mwa
mimea familia ya “Apocynaceae” na unapatikana katika nchi nyingi ikiwemo Kenya,
Uganda, Sudan Kusini,Sudan, Ethiopia, Cameroon, Eritrea, Senegal, Ghana,
Nigeria na Botswana.
Pia
unapatikana katika nchi za Afrika Kusini, Namibia, Guinea, Australia, Cambodia, Japan, Myanmar,
Namibia, Papua, Saudi Arabia, Thailand,Vietnam na Yemen.
Kwa wamaasai mmea huo “Engamryaki “ uchanganywa kwenye
mziwa au supu ya nyama, na mizizi yake imekuwa ikiwekwa kwenye vibuyu
vya kuhifadhia maji ili kuyapa ladha inayovutia.
Jamii nyingine za wafugaji nchini Tanzania kwa
maana ya wasonjo, wagogo, wakurya na wabarbaig zimekuwa zikiutumia mmea huo
kama dawa.
Nchini
Ghana matunda ya mmea huo ambayo ni mazuri na matamu yamekuwa yakitumika kama
kiungo cha kuchochea hamu ya kula kwa wagonjwa, na katika nchi za Kenya na
Sudan umekuwa ukitumika kutengenezea jam.
Mmea
huu wa “Carissa
edulis” unatumika kutibu magonjwa mbalimbali kama vile kifafa,maumivu ya
kichwa, maumivu ya kifua, Kisonono, Kaswende,Kichaa cha mbwa,selimundo,
upungufu wa damu,homa na ngiri.
Magonjwa mengine yanayoweza kutibiwa na mmea huo ni
Kisukari,Presha,kurekebisha mfumo wa Ini,saratani na magonjwa mengine sugu.
Kimsingi mmea huu umetumika kama
tiba miaka elfu iliyopita ambapo katika nchi ya India na maeneo ya jirani umekuwa
ukitibu kuharisha na magonjwa mengine.
Uwendawazimu usioweza kufanyiwa mahesabu na Sir Isaac Newton niliuona pale serikali ya Tanzania ilipokaa kimya
kuona mamia kwa maelfu ya wananchi wake wakiacha kutumia dawa za kisayansi
baada ya kunywa kikombe cha babu.
Tafsiri ya mamia kwa maelfu ya watanzania kufurika kwa babu kupata tiba
ya Kikombe inamaana kuwa Tanzania inawananchi wengi wenye afya dhaifu kwa
magonjwa yasiyokuwa na uhakika wa tiba.
Kikombe cha Babu wa Samunge kuliiumbua serikali ya Tanzania kwa kuionyesha
kuwa inasimamia mfumo dhaifu wa afya na ndio maana watu wake wengi wanahitaji
muujiza wa uponyaji kwa gharama yoyote.
Kwa nini serikali ya Tanzania ilishabikia na kuunga mkono uvumi wa
miujiza ya uponyaji kupitia dawa ya Kikombe cha Babu badala ya kufanya utafiti
wa kutosha kujiridhisha na hali halisi ya kile kilichodaiwa ni muujiza wa
uponyaji.
Swali
la kujiuliza hapa ilikuwaje mmea huo unaojulikana kwa karne kadhaa kama dawa ya kutibu magonjwa mbalimbali
ukapewa sura mpya ya kuwa na maajabu ya kipekee kupitia Kikombe cha Babu wa
Samunge?
Na
kama ni kweli mmea huo ulikuwa na upako na nguvu ya kipekee katika kutibu
magonjwa sugu kama Kisukari, Saratani na UKIMWI, upako na uwezo huo wa
kiuponyaji umeenda wapi kwa sasa?
Serikali ya Tanzania ilijifunza nini kwa kuwa na viongozi wenye afya
dhaifu kama ilivyokuwa kwa wananchi wake ambao mamia kwa maelfu walimiminika
kwa babu ili kupata kikombe kuponya magonjwa yao ambayo yameshindikana kutibiwa
mahali pengine?
Tafsiri nyingine ni kwamba taifa halina mipango, vipaumbele au mkakati
wa makusudi wa kuimarisha afya za watu wake kupitia lishe bora pamoja na huduma bora za afya ndio maana linategemea
miujiza kama ile ya “Kikombe cha Babu.”
Watanzania wengi wanasumbuliwa na magonjwa yatokanayo na tabia ya kula
vyakula na kunywa vitu visivyokuwa na manufaa kwa miili yao na hii inatokana na
udhaifu wa mfumo wa umma katika kutoa elimu sahihi kuhusu lishe bora.
Licha ya uwepo wa mamlaka zinazosimamia mambo ya lishe, kama taifa
hakuna mkakati wa namna gani serikali inataka watu wake wawe na utaratibu
sahihi katika ulaji na unywaji wao ili kujenga taifa la watu wenye afya
madhubuti.
Uduni wa Lishe kwa watanzania unaonekana kwa watu wa matabaka yote,
wasomi, wasio wasomi, wamijini na wavijijini.
Miujiza ya “Kikombe cha Babu”
hata sasa bado inaendelea kwa kuibuka wimbi la watu wanaojiita wataalamu wa
tiba mbadala ambao wengi wao wanautumia
mwanya wa serikali ya Tanzania kutojishughulisha na afya za watu wake.
Na kwa kuwa hiyo ndio hali halisi ujenzi wa uchumi wa kati na Tanzania
yenye viwanda unategemea kujengwa na watu wenye afya za namna gani?
*****************************
No comments:
Post a Comment