Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Monday, December 14, 2015

MAWAKILI NCHINI WATAKIWA KUJITOLEA KUTETEA WATU WASIO NA UWEZO WA KIFEDHA



NA Lucas Raphael,Tabora.

MAWAKILI mkoani Tabora wametakiwa kuwa na moyo wa kujitolea kusaidia wananchi wasio na uwezo wa kifedha ambao wanaokabiliwa na matatizo ya kisheria au ya kijamii yanayohitaji msaada wa kisheria.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili,Tanganyika Law Society-TLS, mkoani Tabora wakili Mussa Kassimu wakati wa maadhimisho ya Siku ya  msaada wa Sheria yaliyofanyika kimkoa katika uwanja wa Stendi ya zamani mjini Tabora.

Alisema zipo jamii zinazokabiliwa na matatizo mbalimbali ya kisheria lakini hazina uwezo wa kuwalipa wanasheria ili waweze kushughulikia matatizo yao kutokana na gharama kuwa kubwa kuwatetea mahakamani.

‘Naomba sana mawakili wenzangu tuwe na moyo wa huruma kwa kujitolea kutoa msaada wa kisheria kwa wenzetu wenye shida mbalimbali na  ambao hawana  uwezo wa kuweka mwanasheria atakayesimamia shauri lake katika vyombo vya sheria’, alisisitiza wakili huyo.

Aidha Mussa aliwasisitiza wananchi kukitumia kitengo cha kutoa msaada wa kisheria pasipo malipo yoyote kwa mwaka mzima kilichopo katika Ofisi za Chama cha Mawakili (TLS) kinachoitwa Legal Action Committee.

Akitoa salamu katika maadhimisho hayo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Amir Mruma aliwataka wananchi  wenye matatizo mbalimbali kujitokeza kukutana na Mawakili kwa lengo la kupata msaada wa kisheria pasipo malipo yoyote.

Aliwataka mahakimu wote kuzingatia maadili ya kazi zao ili kutenda haki katika mashauri yote wanayosikiliza pamoja na kuharakisha usikilizwaji wa mashauri yote ya nyuma na mapya ili kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani.

Aidha Jaji huyo aliwataka wadau wa sheria kutenganisha shughuli za wanaharakati wa sheria (Paralegal) na Wanasheria ikiwemo suala zima la uandaaji nyaraka za kisheria kufanywa na wanasheria na sio vinginevyo.

Aidha amewataka wanasheria kujikita zaidi kwenye sheria na kuachana na  uanaharakati.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni ‘Unyanyasaji wa Kijinsia sasa basi.’

No comments: