Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, December 26, 2015

KANISA LA KCC TABORA LAMPONGEZA RAIS DKT. MAGUFULI

Na Allan Ntana, Tabora

KANISA la Kitete Christian Center (KCC-TAG) la mjini Tabora
limempongeza Rais wa awamu ya tano Dkt.John Pombe Magufuli kwa hatua mbalimbali za kiutendaji alizochukua kulinda maslahi ya Taifa.

Pongezi hizo zimetolewa na Askofu Paul Meivukie wa kanisa hilo
alipokuwa akitoa salamu za Krismasi mara tu baada ya kumalizika kwa
ibada iliyofanyika kanisani hapo.

Alisema utendaji kazi wa Rais Magufuli unapaswa kuungwa mkono na wapenda maendeleo wote kwani ameonyesha dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania kwa kutanguliza maslahi ya taifa kwanza pasipo kuangalia itikadi za kisiasa.

“Rais ameonyesha wazi dhamira yake ya kuleta maendeleo na kile
anachotaka kifanyike anakisimamia kwa vitendo, katika hili
tunampongeza sana na tutaendelea kumwombea awe na afya njema na
hekima katika utendaji wake”, aliongeza.

Aidha Askofu Meivukie alipongeza uamuzi wa Rais wa kufanya maadhimisho ya mwaka huu ya Uhuru wa Tanganyika kuwa siku ya usafi wa mazingira kwa nchi nzima huku akibainisha kuwa usafi ni jambo la muhimu sana kwa ustawi wa jamii na linapaswa kuendelezwa na watendaji wote.

Ili kudumisha amani, upendo na mshikamano katika nchi hii, Askofu
alitoa wito kwa Uongozi wa Serikali ya awamu ya tano kushughulikia
changamoto kadhaa zilizopo ikiwemo suala la uchaguzi wa Zanzibar ili
lisije kuondoa amani iliyopo sasa hapa nchini.


‘Tunapoadhimisha sikukuu hii ya kuzaliwa kwa Yesu Kristu kila mmoja
anapaswa kujichunguza na kujiwekea tumaini jipya la kuingia 2016 akiwa
na Bwana Yesu, hivyo natoa wito kwa Watanzania wote kuendelea
kudumisha amani, upendo na mshikamano’, aliongeza.

Akitoa salamu kwa niaba ya waumini, Mzee  wa kanisani kiongozi Dr. Frank Matimbwa aliwataka Watanzania wote kumpokea Yesu Kristu katika maisha yao kwa kuwa ni mkombozi wa ulimwengu,mfalme wa amani na mshauri wa ajabu.

Aliongeza kuwa Yesu Kristu aliyezaliwa ndiye atakayetungooza kulinda
na kutetea amani tuliyonayo sasa hivi ili kuendeleza ustawi wa kanisa
na nchi kwa ujumla.

No comments: