![]() |
Mkuu wa wilaya ya Tabora Suleiman Kumchaya akiwahutubia wakazi wa kijiji cha Kapunze,kata ya Ikomwa |
Na Paul Christian, Tabora.
Wazazi na walezi wa wilaya ya Tabora wametakiwa
kuwapeleka watoto wao shule na endapo watashindwa kufanya hivyo watachukuliwa
hatua za kisheria.
Mkuu wa wilaya ya hiyo Suleiman Kumchaya ametoa
agizo hilo Jumanne jioni alipokuwa akiwahutubia wakazi wa kijiji cha Kapunze
katika kata ya Ikomwa wilayani humo.
Amesema serikali ya awamu ya tano inatoa elimu
bure kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne na kwamba wazazi au walezi
hawapaswi kuchangia fedha yoyote.
Mkuu huyo wa wilaya ya Tabora amewataka wazazi na
walezi wenye watoto wenye umri wa miaka kati ya minne na mitano kuwapeleka
kuandikishwa kwa ajili ya kuanza darasa la awali mapema mwaka ujao.
Aidha amesisitiza watoto wenye umri wa miaka sita waandikishwe darasa la kwanza na kwamba zoezi hilo
halipaswi kutozwa fedha.
Kumchaya amesema kwa kuwa jukumu la kutoa elimu
bure kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne liko mikononi mwa serikali
hakuna sababu ya mtoto kushindwa kufika shule na kusoma.
Amebainisha kuwa serikali imechukua jukumu la
kugharamia madawati, vifaa vya michezo,chakula kwa wanafunzi wa bweni,ujenzi wa
miundombinu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa na nyumba za walimu.
Mkuu huyo wa wilaya amesema jukumu la wazazi na
walezi ni kuwapatia watoto wao sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia
kama vile kalamu na madaftari, nauli za kuwasafirisha watoto wao wanapotoka na
kurudi shule wakati wa likizo.
Aidha kumchaya ameonya kuwafukuza kazi walimu watakaobainika kuomba fedha wakati wa kuwaandikisha watoto kujiunga
darasa la awali, la kwanza pamoja na kidato cha kwanza.
Ametoa wito kwa wazazi na walezi wilayani humo
kutotoa fedha na endapo watatakiwa kufanya hivyo watoe taarifa ili
hatua za kinidhamu zichukuliwe.
No comments:
Post a Comment