Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, December 26, 2015

WATU SITA WAHUKUMIWA KWENDA JELA MIAKA 30 KWA UNYANG'ANYI WA SILAHA.



Na, Thomas Katobhaya. Tabora.

Mahakama ya hakimu mkazi wa mkoa wa Tabora imewahukumu watu sita kati ya saba kutumikia kifungo cha miaka 30 kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kufanya kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Washitakiwa hao Sadick Lushikama, Sylvester Mussa, Abel Benedikito,
Haji Athuman, Fransincy na Ramadhan Kassim pamoja na kupewa adhabu hiyo bado wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya polisi wawili wa kituo cha
Usoke.

Adhabu hiyo imetolewa wiki hii na hakimu Jackton Rushwela baada ya ushahidi wa utambuzi  ulioungwa mkono na maelezo ya onyo yaliyotolewa  kama kielelezo na upande wa mashitaka uliokuwa unawakilishwa na wakili wa serikali Idd Mgeni.

Katika hukumu yake hakimu Rushwela alisema shahidi wa kwanza ambaye ni miongoni mwa waanga wa tukio hilo aliweza kuwatambua washitakiwa hao hata kwenye gwaride la utambuzi lililoendeshwa na polisi.

Hakimu Rushwela alisema kuwa washitakiwa hao  waliweza kutambuliwa na mashahidi wa kesi hiyo kutokana na mwanga wa taa ya umeme  na baadhi yao waliishi mjini Urambo miaka ya karibuni na kwamba  utetezi wao hauna nguvu kisheria.

Washitakiwa wote katika utetezi wao walidai kwamba hawakuhusika na
kosa hilo bali walikamatwa na polisi kwa nyakati tofauti na kisha
kupigwa sana huku wakilazimishwa waeleze ziliko silaha walipo kataa
walifikishwa mahakamani kujibu shitaka hilo.

Awali wakili wa serikali Idd Mgeni aliiambia Mahakama hiyo kuwa
washitakiwa walitenda kosa hilo Aprili 28/2014 katika kijiji na kata
ya Usoke wilayani Urambo.

Wakili mgeni alidai kuwa siku hiyo majira ya saa mbili usiku
washitakiwa wakiwa na bunduki na mapanga walivamia dukani kwa bwana na bibi Ibrahi Mohamed na kupora fedha taslimu Tshs 6,035,000/= pamoja na simu moja na vocha za Tshs 250,000/=.

Aliongeza kuwa kabla ya unyanganyi huo  washitakiwa walifyatua risasi
hewani kuwatishia majirani wasiweze kufika kutoa msaada.

Wakili Mgeni aliiomba Mahakam itoe adhabu kwa mujibu wa sheria kwa
washitakiwa wote ili liwe ni fundisho kwa wananchi wengine wanashindwa kufanya kazi za kujipatia kipato halali wanajiingiza kwenye uharifu.

Akitoa adhabu hiyo hakimu Rushwela alisema kuwa kwa vile kosa la
unyang’anyi linaangukia kwenye adhabu zenye kikomo zisizokuwa na
punguzo washitakiwa wote watatumikia kifungo cha miaka 30 jela japo
wanayo nafasi ya kukata rufaa.

No comments: