Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, December 26, 2015

WATANZANIA WAASWA KUACHA UVIVU, UZEMBE



Na Allan Ntana, Tabora.

WATANZANIA wameaswa kujiepusha na tabia ya uvivu na uzembe   ili waingie mwaka mpya wa 2016 kwa kishindo wakiwa na dhamira  ya kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo.

Wito huo umetolewa na Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God Mkoa wa Tabora Paul Meivukie katika ibada maalumu ya maadhimisho yasikukuu ya Krismas iliyofanyika usiku wa mkesha wa sikukuu hiyo katika kanisa la Kitete Christian Center mjini Tabora.

Alisema maadhimisho ya sikukuu ya kuzaliwa Yesu Kristu ni fursa pekee kwa kila mwanadamu kuchunguza mienendo yake, tabia, utendaji na uchaji Mungu na kuchukua hatua ya mabadiliko ili kuanza vizuri mwaka mpya.

‘Wito wangu katika krismas hii, tukatae uvivu na uzembe, tudumishe mshikamano wetu na upendano ili mwaka 2016 tuwe na maisha yenye baraka, furaha na amani’, alisema.

Aidha alibainisha kuwa kila mtu anapaswa kuufanya mwaka 2016 kuwa wa kuboresha utumishi wake ili astawi vizuri kiroho na kimwili kwa kuwa aliyezaliwa ni mkombozi, mfalme wa amani na ni mshauri wa
ajabu.

Askofu Meivukie Alinukuu kifungu cha biblia katika kitabu cha Isaya 9: 6 na kusema Yesu alizaliwa ili kuwakomboa wanadamu wote hapa ulimwenguni na wote watakaomsadiki na kuendelea kumtumaini katika maisha yao wataona matendo yake makubwa.

Mwanadamu ana changamoto nyingi za kiuchumi, kifedha, kimwili na kiroho lakini kuzaliwa kwa Yesu Kristu ni tumaini jipya katika maisha yao kwa kujituma katika kila jambo, yeye ni muweza wakimsadiki atawatoa walipo na kuwapeleka kwenye mafanikio  ya kiroho na kimwili katika mwaka 2016, aliongeza.

Aidha aliongeza kuwa aliye na Yesu hatashindwa katika jambo lolote lile kwa kuwa atalindwa na mitego yote ya wabaya, atabarikiwa na kuinuliwa katika maisha yake kiroho na kimwili.

Askofu huyo alisema kuwa Yesu pekee ndiye anayeweza kubadili huzuni za watu kuwa furaha kama wataendelea kujitoa zaidi kwake.

Askofu Meivukie alitoa wito kwa Serikali ya awamu ya tano kutunza amani  kwa kushughulikia changamoto zilizopo sasa hivi na zinazoendelea kujitokeza ikiwemo suala la uchaguzi  wa Zanzibar.

Naye Mzee wa kanisa hilo Kiongozi Dr Frank Mtimbwa alisema kuzaliwa kwa Yesu Kristu kunaleta tumaini jipya katika maisha ya kila mwanadamu hivyo aliwataka waumini hao waendelee kumwamini ili alete mabadiliko katika maisha yao.

No comments: