Na Paul Christian,Tabora.
Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, wilaya ya
Uyui mkoani Tabora Mheshimiwa Almasi Maige amekanusha uvumi unaoenezwa na watu
wasiojulikana kwamba amesimamishwa kujihusisha na shughuli za Bunge kwa muda wa
miezi sita kwa madai ya kuvunja kanuni kwa kuongea na simu ya mkononi akiwa
ndani ya moja ya vikao vya Bunge hilo mjini Dodoma.
Akiongea kwa njia ya simu na mwandishi wa Voice Of
Tabora FM leo asubuhi mbunge huyo amesema hajawahi kusimamishwa na Spika wa
Bunge hilo kwa kinachodaiwa kuvunja kanuni kwa kuongea na simu ya mkononi
akiwa ndani ya ukumbi wa bunge wakati wa mkutano wa kwanza wa Bunge la 10.
Mheshimiwa Maige amefafanua kuwa katika mkutano huo
wa kwanza hakuna mbunge hata mmoja aliyesimamishwa kwa madai ya kuvunja kanani
za Bunge kwa kuongea na simu wakati vikao vikiendelea.
Mbunge huyo wa Jimbo la Tabora Kaskazini amesema, “mimi
sio mgeni wa kanuni za Bunge kwa kuwa nimekuwa mbunge wa Bunge la Katiba la
mwaka 2014, hivyo nafahamu na kuzielewa kanuni vizuri.”
Aidha Mheshimiwa Maige amekanusha uvumi kuhusika
na biashara ya utoroshaji wa makontena kutoka bandari ya Dar es Salaam na kukwepa
kulipa ushuru kwa kuwa yeye si mfanyabiashara wa makontena.
Amesema, “mimi si mfanyabiashara wa makontena,
biashara yangu ni ya mawasiliano na ulinzi wa kisasa wa kufunga mitambo.”
Mheshimiwa Maige amewataka wananchi wa Jimbo la
Tabora Kaskazini kuwapuuza watu hao wanaovumisha mambo yasiyofaa kwa malengo
wanayoyajua wao ambayo hayana maslahi kwa wananchi wa jimbo hilo.
Amebainisha kuwa uvumi huo unatungwa na kusambazwa
na watu wasiokuwa na busara na kwamba watu hao wanapaswa kutambua uchaguzi
umekwisha na sasa ni wakati wa kuchapa kazi.
Mheshimiwa Maige amebainisha kuwa kwa sasa yuko
jijini Dar es Salaam akiendelea na zoezi la utafiti kuhusu matatizo
yanayolikabili zao la tumbaku na kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo, zoezi
ambalo amelianza mara baada ya kuahirishwa kwa mkutano wa kwanza wa Bunge la
10.
Amesema katika utafiti wake wa awali alifanya
ziara ya kutembelea wadau wa zao la Tumbaku mkoani Tabora ambao ni makampuni
yanayonunua tumbaku, Bodi ya Tumbaku TTB, mlajisi wa vyama vya Ushirika pamoja
na taasisi za fedha.
Mheshimiwa Maige ameeleza kuwa akiwa
jijini Dar es Salaam anaendelea na utafiti huo ambao utasaidia kukabiliana na
changamoto za kilimo cha tumbaku ambacho kimekuwa kikilalamikiwa kwa kukosa
tija na wakulima wa zao hilo jimbo la Tabora Kaskazini.
Amesema, “hauwezi kuongelea Tabora bila ya
Tumbaku, bila ya wadau wa Tumbaku.”
Mkutano wa kwanza wa Bunge la 10 ulianza tarehe 13
hadi 20 Novemba, 2015 ambao ulikuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo kuchaguliwa
kwa Spika wa Bunge na baadaye kuapishwa,
kuapishwa kwa wabunge, kuthibitisha uteuzi wa waziri mkuu, kuchaguliwa kwa
Naibu Spika na hatimaye Rais Magufuli kulihutubia na kulizindua Bunge.
No comments:
Post a Comment