Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, December 26, 2015

HOSPITALI YA KITETE YAKABILIWA NA UPUNGUFU WA DAWA ZA KIFAFA




Na, Rehema Cleophace,Tabora.
  
Idadi ya watu wanaougua ugonjwa wa kifafa na kupelekwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Tabora Kitete inaendelea kuongezeka kuliko magonjwa mengine ya akili mkoani hapa.

Afisa muuguzi msaidizi wa magonjwa ya akili katika hospitali ya Kitete bibi Suzan Msagata amesema idadi ya wagonjwa hao imeongezeka mara mbili kwa mwaka huu kutokana na upungufu wa dawa za ugonjwa huo unaoikabili hospitali hiyo.

Amesema hali ya upungufu wa dawa unasababisha idadi ya wagonjwa kuongezeka kutokana na kutopatiwa matibabu ya kutosha na hali ya kuumwa kujirudia.

Afisa muuguzi huyo amesema mwaka huu zaidi ya wagonjwa 600 wametibiwa katika hospitali hiyo na kuruhusiwa na kwamba waliolazwa kwa mwaka huu ni wagonjwa 30.

Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kitengo hicho cha magonjwa ya akili bibi Msagata amesema tatizo la kukosekana dawa limekuwa sugu hivyo ameitaka serikali kuhakikisha inatoa dawa za kutosha ili wagonjwa watibiwe kwa kupewa dawa za muda mrefu kwa lengo la kuepuka ugonjwa kujirudia rudia.

Ameitaja changamoto nyingine kuwa ni jamii kuuhusisha ugonjwa wa kifafa na imani za kishirikina hali inayosababisha wagonjwa kuongezeka kutokana na wengi wao kuamini kuwa mgonjwa wao karogwa hivyo kuchukua uamuzi wa kumpeleka kwa mganga wa kienyeji.

Kutokana na hali hiyo muuguzi huyo msaidizi amewasihi wananchi kuachana na imani hiyo badala yake wawapeleke wagonjwa wa kifafa hospitalini kwa matibabu ambayo hutolewa bure.

No comments: