Na Lucas Raphael,Igunga.
Mwalimu mmoja anayefundisha shule ya Sekondari
Igunga Day iliyopo wilayani Igunga mkoa wa Tabora anatuhumiwa kutoroka na fedha
za wanafunzi wa shule hiyo zilizochangwa kwa ajili ya kuwawezesha kufanya ziara
ya masomo katika hifadhi ya Ngorongoro.
Mwalimu huyo Paulo Msabila anadaiwa
kuwachangisha wanafunzi hao Tshs. 50,000/= kila mmoja kwa lengo la kutembelea
hifadhi hiyo yenye umaarufu wa kipekee Duniani.
Akizungumzia tukio hilo mmoja wa wazazi wa
wanafunzi hao Rashid Mgendi alisema alitoa Tshs 50,000/= kwa ajili ya mtoto wake
Juma Rashid anayesoma kidato cha pili katika shule hiyo ili aweze kushiriki
ziara hiyo ya mafunzo iliyoyeyuka bila maelezo.
Joseph Nyangi ni mzazi wa mwanafunzi Bahati
Marwa anayesoma kidato cha tatu ambaye alitoa kiasi cha Tsh 50,000/= kwa ajili
ya kumuwezesha mtoto wake kwenda kujifunza katika hifadhi hiyo ya Ngorongoro alishangazwa
na kitendo cha mwalimu huyo kutoweka na fedha zao.
Wazazi hao walisema kuwa baada ya kuona ziara
hiyo ya mafunzo imeshindikana walikwenda kumuona mwalimu huyo ili arejeshe
fedha walizochanga lakini mwalimu huyo hakufanya hivyo hadi shule hiyo imefungwa
kwa likizo.
Aidha mwalimu huyo hajulikani alipo na
hata simu yake ya mkononi haipatikani licha ya kutafutwa kwa zaidi ya wiki
moja.
Mkuu wa shule hiyo ya sekondari Igunga day
,Nelson Edward alikiri kuwa mwalimu huyo aliwachangisha wanafunzi wa
shule hiyo zaidi ya shilingi milioni 2.8 ambazo hakuzitumia kwa lengo lililokusudiwa
na badala yake alizitumia kujinufaisha.
Kaimu afisa elimu sekondari wilayani Igunga Fred
Matalu amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba ameitaka bodi ya shule hiyo
kuchukua hatua.
No comments:
Post a Comment