Na Halima Ikunji, Tabora.
Kampuni ya Ujenzi ya SARAM ya jijini Dar es Salaam
inakusudia kuifikisha mahakamani halmashauri ya wilaya ya Kaliua mkoani Tabora
kwa kuvunja mkataba wa ujenzi bila makubaliano ya pande mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tabora
meneja wa kampuni hiyo Raymond Mkandawile amesema aliingia mkataba na
halmashauri hiyo ya kujenga nyumba nne za watumishi, jengo la wagonjwa wa nje la
hospitali ya wilaya OPD,ofisi ya mkurugenzi pamoja na jengo la maonesho ya nane
nane katika mtaa wa Ipuli mjini Tabora.
Meneja huyo amesema mkataba wa kujenga majengo
hayo umevunjwa na halmashauri hiyo huku wakiwa wanaidai jumla ya shilingi milioni
234.
Mkandawile alifafanua kuwa katika ujenzi wa OPD
wanadai Tsh. Mil.110, nyumba nne za watumishi Tsh. Mil. 54 na jengo la ofisi ya
mkurugenzi Tsh. Mil 70.
Alisema, “tumesikitishwa sana na uamuzi wa kikao
cha madiwani wa halmashauri hiyo kilichokaa mwezi huu na mkurugenzi wa
halmashauri hiyo Athumani Kihami kutangaza kuvunja mkataba na kampuni yetu kwa
madai tumekiuka mkataba jambo ambalo si kweli.”
Mkandawile ameeleza kuwa kitendo hicho cha halmashauri ni udhalilishaji wa kampuni ya SARAM ambayo imejenga majengo hayo kwa asilimia 99, isipokuwa halmashauri hiyo iliingia kwenye nyumba hizo nne pasipo makabidhiano ya aina yoyote.
Mkandawile ameeleza kuwa kitendo hicho cha halmashauri ni udhalilishaji wa kampuni ya SARAM ambayo imejenga majengo hayo kwa asilimia 99, isipokuwa halmashauri hiyo iliingia kwenye nyumba hizo nne pasipo makabidhiano ya aina yoyote.
Aidha amesema kuwa kilichotokea katika maeneo ya
ujenzi walisimamisha ujenzi kutokana na
halmashauri hiyo kuchelewesha malipo hali iliyosababisha wafanyakazi wa kampuni
hiyo kushindwa kulipwa stahiki zao kwa wakati.
Meneja huyo alikanusha madai kuwa kampuni yake
iliitwa mara kadhaa kwenye vikao vya mazungumzo kujadili kuhusu mkataba wa huo
na haikutuma mwakilishi.
“Hatujawahi kupokea barua yoyote ya wito kutoka
katika halmashauri hiyo kwa lengo la mazungumzo.”Amesema meneja huyo.
Awali mwenyekiti wa halmashauri hiyo Haruna Kasele
alisema kampuni hiyo iliitwa zaidi ya mara tatu katika meza ya mazungumzo lakini
haikutokea, ndipo baraza la madiwani likaridhia kuvunjwa kwa mkataba huo.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kaliua Magdalena Sakaya
amemtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuwapa madiwani mkataba huo uliovunjwa
ili waupitie na kubaini kiini cha mgogoro huo.
Amemtaka mkurugenzi huyo
kutotangaza upya tenda ya ujenzi wa majengo hayo hadi pale madiwani
watakapojiridhisha baada ya kuupitia mkataba huo.
No comments:
Post a Comment