Na Paul Christian, Ulyankulu.
Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu wilaya ya Kaliua
mkoani Tabora Mheshimiwa John Peter Kadutu ameahidi kuboresha mazingira ya
makumbusho ya Mtemi Milambo yaliyopo katika eneo la Ikonongo.
Akizungumza mbele ya familia ya Mtemi Milambo
mbunge huyo alisema viongozi wengi wamekuwa wakiahidi kuboresha mazingira ya
Makumbusho hayo lakini wameshindwa kufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali
ikiwemo mambo ya kisiasa.
Kadutu alibainisha kuwa eneo hilo la Makumbusho
linapaswa kuboreshwa ili lilingane na hadhi ya Mtemi Milambo tofauti na
ilivyosasa eneo hilo haliendani na heshima ya Mtemi huyo maarufu.
Aidha alizitaka serikali kuu na halmashauri ya
wilaya ya Kaliua zianze kutambua na kuona umuhimu wa kuwaenzi watemi mbalimbali
ambao waliongoza mapambano ya kupinga ukoloni.
Mbunge huyo alitoa wito kwa wadau mbalimbali
kuungana kwa pamoja ili kutimiza azma ya kuboresha mazingira yanayozunguka
Makumbusho ya Mtemi Milambo pamoja na watemi wengine waliomtangulia.
Mheshimiwa Kadutu alianisha baadhi ya faida
zitakazojitokeza baada ya kuliboresha eneo hilo kuwa ni kuwavutia wageni wengi
zaid wa ndani na nje ya Tanzania kufanya utalii ambao utakuza uchumi na kutoa
ajira kwa wakazi wa jimbo la Ulyankulu.
Awali akisoma taarifa ya Makumbusho hayo afisa
tarafa wa tarafa ya Ulyankulu John Chitanda alisema jamii inayoishi kuzunguka
makumbusho hayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa shule,
zahanati, barabara na visima virefu vya maji.
Eneo la Makumbusho ya Mtemi Milambo lipo katika
eneo la kijiji cha Usigala barabara ya 44 katika jimbo la Ulyankulu na mtemi
huyo alifariki mwaka 1884.
No comments:
Post a Comment