Tarehe 8 Mei 1972, ndege hiyo aina ya Boeing 707 -329 ikiongozwa
na rubani muingereza Reginald Levy ilitekwa nyara na watekaji wanne kutoka
kundi lililojulikana “Black September.”
Utekaji huo ulipangwa na Ali Hassan Salameh na
kuwahusicha watekaji wanne wawili wanaume na wawili wanawake wakiwa na silaha
aina ya bastola wakiongozwa na Ali Taha.
Dakika 20 baada ya kuondoka kwenye uwanja wa kimataifa wa
Wien-Schwechat jijini Vienna,
Austria ,watekaji wakavamia chumba cha
marubani.
Nahodha wa ndege hiyo Levy alisikika akiwaambia abiria 90
“tumepata marafiki” huku yeye mwenyewe na abiria wakisubiri amri kutoka kwa
watekaji hao.
Jambo moja la kuvutia katika tukio hilo mke wa rubani
huyo kiongozi alikuwa miongoni mwa abiria ndani ya ndege hiyo.
Baada ya kuhakikisha wameidhibiti ndege hiyo watekaji
waliwatenganisha abiria wenye asili ya Israel na raia wengine, kisha wakawaelekeza
waende sehemu ya nyuma ya ndege.
Ndege hiyo ikiwa na abiria 94 wakiwemo watekaji hao wanne
ilitua kwenye uwanja wa Lod Airport ambao kwa sasa unajulikana Ben Gurion
International Airport jijini Tel Aviv nchini Israel.
Wakiwa kwenye ardhi ya Israel Watekaji hao walitoa madai
yao kwa serikali ya Israel ya kutaka kuachiliwa huru kwa wafungwa 315 wa
kipalestina ambao walifungwa nchini humo kwa makosa ya Ugaidi.
Katika hali taharuki huku watekaji wakilia na
kukumbatiana kama ishara ya kuagana, nahodha wa ndege hiyo Levy aliweza kutuma
ujumbe kwa serikali ya Israel akiomba msaada wa kuokolewa.
Waziri wa ulinzi
wa Israel Moshe Dayan akafanya mazunguzo na watekaji hao wakati huo huo akifanya mipango ya kijeshi ya kuwaokoa mateka
hao katika operesheni iliyopewa jina la ISOTOPE.
Tarehe 9 Mei, 1972 majira ya saa kumi jioni operesheni ya
kuwaokoa mateka ikaanza ambapo timu ya makomandoo 16 wa kikosi cha Sayeret
Matkal wakiongozwa na Ehud Barak na Benjamini Netanyahu waliikaribia ndege hiyo
iliyotekwa.
Viongozi hao wa operesheni ISOTOPE baadae walishika wadhifa wa uwaziri mkuu wa
Israel ambapo Benjamini Netanyahu ndio waziri mkuu wa sasa wa nchi hiyo.
Makomandoo hao wakiwa wamevalia maovaroli ya rangi nyeupe
walijifanya mafundi wa ndege na kuwashawishi watekaji waamini kuwa ndege hiyo
ilihitaji matengenezo.
Makomandoo hao wakaivamia hiyo ndege na kuidhibiti ndani
ya dakika 10 ambapo waliwaua watekaji wawili wanaume na kuwaweka chini ya
ulinzi watekaji wawili wanawake.
Abiria wote waliokolewa, watatu kati yao walijeruhiwa
ambapo mmoja wa majeruhi hao baadae alipoteza maisha, Benjamini Netanyahu
alipigwa risasi begani katika operesheni hiyo.
Wale mateka wawili wanawake walihukumia kifungo cha
maisha jela lakini baadae waliachiwa huru katika mpango wa kubadilishana
wafungwa baada ya vita ya Lebanon ya
mwaka 1982.
Ndege hiyo
iliyotekwa iliendelea kufanya kazi kwa miaka mitano chini ya shirika la SABENA
kabla ya kununuliwa na jeshi la Israel, ambapo ilibadilishwa matumizi na kuwa
ndege ya kipelelezi kwa miaka mingi.
Nahodha wa
ndege hiyo Reginald Levy alikuwa ni
askari wa kikosi cha anga cha Uingereza ambapo alishiriki kuishambulia
Ujerumani katika vita ya pili ya Dunia na alijiunga na shirika la ndege la
Ubelgiji SABENA mwaka 1952.
Alistaafu kazi
ya urubani mwaka 1982 na akiwa nyumbani kwake Dover alifariki kwa ugonjwa wa saratani tarehe 1 Agosti, mwaka 2010.
Wakati wa tukio
la kutekwa kwa ndege aliyokuwa akiingoza alikuwa akisheherekea siku yake ya
kuzaliwa ya mara ya hamsini.
0684 329 990,paulkagenzi@yahoo.com
No comments:
Post a Comment