Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Wednesday, December 9, 2015

MKURUGENZI KALIUA AMTIMUA MKANDARASI



Na Hastin Liumba, Kaliua

MKURUGENZI mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua mkoani Tabora Athuman Kihamia amevunja mikataba yote ya ujenzi iliyokuwa inatekelezwa na kampuni ya SARAM ya jijini Dar es salaam kwa kushindwa kutimiza matakwa ya  mikataba.

Akitoa taarifa kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo mkurugenzi huyo alisema kuvunjwa kwa mikataba hiyo kunatokana na ukiukwaji wa makubaliano kwa kuchelewa  kukamilisha miradi iliyokuwa ikitekelezwa na kampuni hiyo ndani ya wakati.

Kihamia ailitaja miradi minne  iliyokuwa inatekelezwa na mkandarasi huyo kuwa ni ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na ujenzi wa nyumba nne za watumishi wa halmashauri  na jengo la maonyesho ya nane nane lililopo Mtaa wa Ipuli katika Manispaa ya Tabora.

Alisema kitendo cha mkandarasi huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano kimeisababishia hasara kubwa halmashauri hiyo ikiwemo kupandishiwa kodi ya pango la ofisi za halmashauri jambo lililowashinda  na kuamua kuhamishia ofisi katika nyumba za watumishi.

Aidha alisema uamuzi wa kufutwa kazi mkandarasi huyo ulifuata taratibu zote za kisheria za utoaji zabuni na kikao kilichofikia uamuzi huo wakati baraza la madiwani halipo kilifanya hivyo kwa dhamira njema pasipo uonevu.

Kihamia alifafanua zaidi kuwa mkandarasi huyo alikuwa akilipwa fedha za mapato ya ndani ya halmashauri kwa kila hatua ya ujenzi na kwamba mpaka sasa hadai fedha yoyote na mchakato wa kutafuta mkandarasi mwingine unafanyika.

Akifafanua sakata hilo  Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Serikali za Mitaa Natalis Linuma alisema mkandarasi huyo alishaitwa mara nyingi katika vikao husika lakini hakufika na kusisitiza kuwa suala la kumsimamisha lilikuwa ni jema.

Naye mwanasheria wa sekretarieti ya  mkoa, Richard Lugomela alieleza wazi kuwa suala la mkandarasi huyo lilifuatiliwa kwa kina na kubainika ana upungufu wa mambo mengi  ikiwemo kutoonekana eneo la kazi kwa muda mrefu na kutowalipa wafanyakazi wake hali iliyofanya kazi kuzorota.





No comments: