Na Elias Shija, Uyui.
Wafanyabiashara
wa kata ya Bukumbi wilaya ya Uyui mkoani Tabora wamechanga kiasi cha Tsh. 3,400,000/=
kwa ajili ya kukarabati jengo la kituo kidogo cha polisi cha kata hiyo.
Akizungumzia
suala hilo katibu wa umoja wa wafanyabiashara hao Maziku Kanati amesema fedha
hizo zimetumika kukarabati jengo hilo ili kuimarisha ulinzi katika kukabiliana
na matukio ya mara kwa mara ya uhalifu katani humo.
Amesema
ongezeko la matukio ya uhalifu dhidi ya watu na mali zao yamepelekea wafanyabiashara
hao kujitoa kwa hali na mali kukarabati jengo hilo ili liwe na sifa zinazokubalika
na kuwawezesha polisi kutimiza majukumu yao kikamilifu.
Kanati
amebainisha kuwa hali hiyo itawasaidia kudumisha amani na utulivu wakati wakijishughulisha
na shughuli mbalimbali za kijamii na uzalishaji mali.
Naye
mwenyekiti wa wafanyabiashara hao Jonas Mheza amesema kuimarika kwa kituo hicho
cha polisi kutasaidia kuongezeka kwa askari wanaotoa huduma katika maeneo yao.
Aidha
amesema matukio ya kihalifu katani humo yamekuwa yakitokea mara kwa mara hali
inayowasababisha baadhi ya wafanyabiashara kuwa na hofu kufanya uwekezaji wenye
tija.
Mwenyekiti
huyo amewataka wafanyabiashara na wananchi wa kata ya Bukumbi kutoa ushirikiano
kwa jeshi la polisi katika kuwafichua wahalifu ili wachukuliwe hatua za
kisheria.
Hata
hivyo baadhi ya wakazi wa kata hiyo wamemuomba kamanda wa polisi mkoa wa Tabora
kuwaondoa askari waliowahi kufanya kazi katika kituo hicho siku za nyuma kwa
kuwa hawana rekodi ya uadilifu katika kutekeleza majukumu yao.
No comments:
Post a Comment