TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Eng.
John Ndunguru kukamilisha uchunguzi wake na kumpatia taarifa ya maandishi juu
ya tuhuma ubadhirifu wa fedha za umma unaohusisha uuzwaji wa jengo la KIGODECO
na viwanja 12 vya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambao unadaiwa kukiuka taratibu.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatano, Desemba
30, 2015) kwenye ukumbi wa NSSF, mjini Kigoma wakati akizungumza na viongozi na
watendaji mbalimbali wa mkoa huo alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya
siku mbili mkonai humo.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema anazo taarifa kuwa
jengo hilo liliuzwa kwa sh. milioni 370/- pamoja na jengo jingine la MIBOS kwa
sh. milioni 50/- licha ya kupewa barua na Mkuu wa Mkoa huo kusitisha uuzwaji wa
jengo pamoja viwanja hivyo, bado liliuzwa.
“Katibu Tawala
wa Mkoa kaa na Mkurugenzi wa Manispaa, Mhandisi wa Manispaa na Mhasibu na
unipatie taarifa kwa maandishi ifikapo Jumamosi hii,” alisema Waziri Mkuu huku
akishangiliwa.
“Nataka kujua
nani alifanya tathmini ya jengo, ni kwa nini jengo liliuzwa kwa thamani hiyo,
je ndiyo thamani halisi ya jengo? Ni kwa nini RC alipozuia, utaratibu
uliendelea? Je, utaratibu wa uuzaji ulifuatwa? Ni kwa nini viwanja viliuzwa
chini ya thamani,? Katibu Tawala kaa na watu wako na uniletee hiyo taarifa kwa
maandishi. Tukigundua kuna mianyamianya tutachukua hatua za kinidhamu,” alisema.
Viongozi
walioagizwa kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa ni Mkurugenzi wa Manispaa, Eng.
Boniface Nyambele; Mhandisi wa Manispaa, Eng. Boniface William na Mhasibu wa
Mapato wa Manispaa, Ndg. Bawili Mkoko.
Kuhusu uuzwaji
wa jengo na viwanja, imebainika kuwa Mkuu wa Mkoa huo, Luteni Kanali (Mst),
Issa Machibya alizuia uuzaji huo kwa barua ya tarehe 16 Juni 2015 akitaka
viwanja hivyo vitumike kwa matumizi ya manispaa na mchakato huo usitishwe hadi
mwakani lakini agizo lake lilipuuzwa na jengo likauzwa kwa sh. milioni 370
ambayo ni bei ya kiwanja pekee.
Tuhuma
nyingine zinazopaswa kuchunguzwa ni pamoja na matumizi ya sh. milioni 809 kwa
ajili ya ujenzi wa maabara. Kiasi hicho kilitolewa kutoka kwenye fedha za
miradi ya maendeleo (Capital Development Grants-CDG), Mradi wa Programu ya
Kuendeleza Sekta ya Kilimo na Mifugo (ASDP), Mradi wa Uendelezaji Miji
(Tanzania Strategic Cities Programme –TSCP) na Miradi ya Maendeleo ya Elimu ya
Sekondari (SEDP).
Inadaiwa
kwamba Mkurugenzi huyo kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa idara ya
mipango na fedha walitumia ujenzi wa maabara kama kigezo cha kuchota fedha hizo
bila kutoa taarifa kwa wakuu wa idara husika ambao walikasimiwa fedha hizo.
Tuhuma
nyingine ni manunuzi hewa ya vipuri (spare parts) vyenye thamani ya sh. milioni
8 na manunuzi hewa ya stationeries yenye thamani ya sh. milioni 4.6/-. Haya
yanadaiwa kufanywa Julai 25, mwaka huu na Mkurugenzi huyo akishirikiana na
Mhasibu Mkoko.
Waziri Mkuu
amerejea jijini Dar es Salaam mchana huu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, DESEMBA 30, 2015.
No comments:
Post a Comment