Featured Post

KITUMBO:MAWASILIANO MADHUBUTI YA KIUTAWALA NI SIRI YA MAFANIKIO

Na Paul Christian, Tabora. Mawasiliano mazuri ya kiutawala baina ya wenyeviti na watendaji wa mitaa na wananchi ni jambo muhimu kat...

Saturday, December 26, 2015

JINA LA RAIS MAGUFULI LATUMIKA KUTAKA KUTAPELI WANANCHI KALIUA



Na Hastin  Liumba,Kaliua 

JINA la Rais John Pombe Magufuli limetumika kutaka kuwatapeli fedha
wananchi wa kata ya Zugimlole wilaya ya Kaliua mkoa wa Tabora.

Mtendaji wa kata ya Zugimlole, Miraji Kalangula alibainisha hayo baada ya  kubaini barua inayoelekeza kuwa Rais amebariki wananchi wanaodaiwa kuishi kwenye maeneo ya hifadhi kuendelea kuishi katika maeneo hayo baada ya  kuchangia sh 20,000 kwa kila kaya.

Alisema barua hiyo pia ilieleza kuwa wananchi hao wangepatiwa vitambulisho vya BVR ili kuhalalisha ukaaji wao katika maeneo hayo.

Mtendaji  huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa aliibani nia hiyo ya utapeli kupitia barua iliyokuwa kwa wananchi wa kitongoji cha Iga katika kata hiyo ya Zugimlole.


Alisema barua hiyo iliandikwa tarehe mosi mwezi huu yenye kichwa cha habari ‘mchango wa upigaji picha na kutoa vitambusho kwa mfumo wa BVR kwenye maeneo yaliyokuwa hifadhi’.

Alieleza kuwa barua hiyo yenye kumbukumbu namba KDC/TB. 07/2/057/03,namba za simu 0686674621 na nukushi 0732988451  ilihusisha ofisi ya mkuu wa wilaya na halmashauri ya wilaya Kaliua mkoa wa Tabora na kuhusisha sahihi ya aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo Saveli Maketa.

Kalangula alieza kuwa barua hiyo ilisomeka “Rais John Pombe Magufuli
ameachilia huru maeneo ya hifadhi za taifa ambayo wananchi walikuwa
wamevamia hivyo wanatakiwa walipe kila kaya sh 20,000 ili waendelee
kuishi na kupatiwa  vitambulisho kupitia mfumo wa BVR.”

Aliongeza kuwa barua hiyo ilielekeza “wananchi hao watakapolipa fedha hizo afisa anayesimamia michango hiyo atawaletea stakabadhi.”

Mtendaji huyo alibainisha kuwa maeneo yanayodaiwa kuwa ndani ya hifadhi ni Stesheni za Uyumbu,Kangeme,Lumbe,Usinge hadi mpakani mwa wilaya ya Kaliua na Mpanda.

Aidha Barua hiyo ilieleza kuwa hilo ni tamko la Rais alipokuwa akifunga Bunge la 11 la jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma.

Alisema barua hiyo iliwataka mwenyeviti wa serikali za vijiji  kupitia
kila familia na kukusanya michango hiyo.

Alibainisha kuwa barua hiyo ilisisitiza  kuwa zoezi hilo ni la wiki moja na michango ingeanza kukusanywa kuanzia tarehe 3 hadi 12 Disemba,2015 na kwamba wananchi wahakikishe majina yao yameandikwa kwenye daftari.

Mtendaji huyo alisema barua hiyo ilieleza kuwa majina ya wote waliochangia yatapelekwa kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya na baadaye kuletewa stakabadhi zao  ili zoezi lianze mara moja.

Kalangula aliongeza kuwa barua hiyo ilitoa onyo kwa yeyote atakayekaihidi agizo la serikali adhabu kali itatolewa dhidi yake na
kupelekwa polisi Kaliua na Lumbe ikiwemo ofisi ya halmashauri ya
wilaya a Kaliua.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua Athuman Kihamia alikana kuitambui barua hiyo wala kufanya maamuzi dhidi ya wananchi hao waliovamia maeneo ya hifadhi
hivyo barua hiyo ni utapeli mtupu.

Alisema anaifanyia uchunguzi barua hiyo ili kuchukua hatua dhidi ya
wahusika wote walitumia jina la Rais kutaka kutapeli wananchi.

Meneja wa misitu wilaya ya Kaliua John Alex Madohora alisema barua
haina uhalali wowote isipokuwa ni kikundi cha watu matapeli ambao
walitaka kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na wao wanafanya
uchunguzi ili kuwabaini wahusika.

Mkuu wa wilaya ya Kaliua Hadija Nyembo alisema barua hiyo ofisi yake
haiitambui na wanafanya uchunguzi ili kuchukua hatua dhidi ya wahusika wote.

Barua hiyo ina muhuri na sahihi ya aliyekuwa mkuu wa wilaya
aliyehamishiwa wilaya ya Kigoma Saveli M. Maketa.

No comments: