Na Nicholaus Kagusa, Tabora.
Wakulima wa kijiji na kata ya Malolo katika Manispaa
ya Tabora wamesema ucheleweshwaji wa pembejeo za ruzuku umesababisha wakulima
wasio na uwezo kushindwa kufikia malengo
ya kilimo chenye tija.
Mkulima wa kijiji hicho Khadija Mdemi amesema
pembejeo hizo zimechelewa kufika ambapo mbegu na mbolea za kupandia zimefika
wakati mimea ya mahindi imekwisha ota.
Mkulima huyo amebainisha kuwa vocha za pembejeo
hizo zinawafikia wakulima wachache ukilinganisha na idadi ya kaya masikini
zinazohitaji kujikwamua kupitia kilimo.
Naye Tilizo Kasto mkulima wa kijiji cha Malolo
amesema kuwa mara kadhaa mbegu za kisasa zinazotolewa kwenye mpango huo zimekuwa
hazioti jambo lililomgharimu kutafuta mbegu za mahindi aina nyingine.
Mkulima huyo pia ameeleza kuwa mara nyingi mifuko
ya mbolea pamoja na mbegu inawafikia ikiwa na ujazo pungufu kutokana na hujuma.
Akizungumzia hali hiyo mwenyekiti wa kamati ya
Vocha yenye wajumbe sita katika kijiji hicho Rehema Lukaya amesema upungufu wa
mbolea na mbegu za ruzuku zinazotolewa kwa wakulima hao unatokana na baadhi yao
kuziuza kwa watu wenye uwezo na hivyo kupoteza maana halisi ya mpango huo.
Afisa mtendaji wa kijiji hicho ambaye pia ni afisa
pembejeo wa kata ya Malolo Paulo Thobias Suwi amesema wakala aliyepewa
kandarasi ya kusambaza pembejeo hizo ni
John Mchele Enterprises na kwamba alianza kufikisha pembejeo hizo mnamo Novemba
27 mwaka huu.
Kutokana na kauli hiyo ya Afisa mtendaji ni
dhahiri kuwa Novemba 27 ni muda ambao wakulima wengi walikuwa wamepanda mahindi
katika mashamba yao hivyo mbegu na mbolea za kupandania zilichelewa kuwafikia
wakulima hao.
Aidha Paulo alifafanua kuwa wakala huyo kabla ya
kukabidhi pembejeo huwa anaipima mifuko ya mbolea na mbegu ili kuhakikisha
ujazo wake tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
Meneja wa kampuni ya John Mchele Enterprises Juma
Abdallah amesema wamepewa kandarasi ya kusambaza pembejeo hizo katika kata tatu
za Malolo, Itetemia na Kabila na wamekuwa wakijitahidi kuwahisha pembejeo kwa
wakulima.
Amesema kampuni yake pia inalojukumu la kuhakikisha
ujazo wa mbolea na mbegu uko sawa kulingana na maelezo ya mkataba kabla ya kuwakabidhi
wakulima.
Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora
Ditirick Mwinuka amesema mpango wa pembejeo za ruzuku unaotoa mbolea za
Minjingu, UREA, DAP, CAN pamoja na mbegu za mahindi aina chotara na kwamba unahudumia vijiji 11 katika manispaa hiyo.
Amesema Halmashauri hiyo ilifanya makadirio ya
vocha 5,000 lakini ikapokea vocha 1,312 sawa na kaya 11,000.
Mwinuka amebainisha kuwa mpango huo unagusa kaya
masikini ambazo hujengewa uwezo kwa kupewa pembejeo hizo kwa muda wa miaka
mitatu mfululizo kabla ya mpango huo kuhamia kwa kaya nyingine masikini.
No comments:
Post a Comment